Thursday, November 15, 2012

waweza inazindua kampeni mpya kuchochea umma kuchukua hatua

Ni Sisi yahamasisha utashi wa wananchi
Twaweza inazindua kampeni mpya kuchochea umma kuchukua hatua
 
Dar es Salaam, 15 Novemba 2012: Twaweza inazindua kampeni mpya inayohamasisha fikra kwamba wananchi wanaweza kujiletea mabadiliko wenyewe, badala ya kusubiri serikali, wanasiasa, wafadhili au AZISE kuwafanyia kila kitu.Taasisi ya Twaweza inaamini kwamba kwa kuamua na kuchukua hatua, wananchi kote Afrika ya Mashariki wanaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kudumu na kuweka msukumo kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe.

Kauli mbiu hiyo ya kampeni iliyo katika lugha ya Ki-Swahili inaweza kufasiriwa kama ‘Mabadiliko ni mimi. Ni wewe. Ni sisi.’ Lengo ni kutoa msukumo kwenye midahalo na kuchukua hatua katika dhana hii ya ‘Ni sisi’, kuhusu namna gani tunaweza kutoa mchango kwa jamii, maendeleo na maisha yetu. Yanayozungumzwa kwenye kampeni hiyo yanatokana na hali halisi ya maisha ya watu na kumpa changamoto kila mwananchi ili afikiri kuhusu masuala haya na kujitafutia suluhu kwa matatizo wanayokabiliana nayo.

Kampeni itahusisha shughuli mbalimbali nchini Tanzania, Kenya na Uganda. Kazi kuu ni matangazo sita ya televisheni kuhusu utumishi wa umma (PSAs). Kila tangazo la umma litamwonyesha mtu mmoja jasiri anayechukua hatua madhubuti au ile isiyo ya kawaida ili kulikabili tatizo fulani na, kwa kufanya hivyo, anawatia hamasa wengine kujiunga naye. Kisha kwa pamoja wanaleta mabadiliko katika jamii yao.

Kampeni hiyo pia itahusisha vipindi vya redio, machapisho, masuala yasiyozoeleka sana na yale yanayotazama mbali zaidi ya taratibu za kawaida. Twaweza inashirikiana na washirika kadhaa ili kutayarisha vipindi vya majadiliano, katuni, video za muziki na maonyesho ya barabarani, sambamba na matangazo ya utumishi wa umma kupitia majukwaa haya mbalimbali. Shughuli zote hizi zinalenga kusukuma wazo kuu la mabadiliko yanayoletwa na wananchi wenyewe.

Kiini cha ujumbe wa kampeni ni kuonyesha jinsi gani sote katika jamii tunavyohusiana – kile kinachotuunganisha.Kwa upande mmoja, tunaweza kujichukulia kwamba sisi ni tofauti na serikali na watendaji wa umma, au tunaweza kujiona kama washiriki kwenye uwajibikaji ili kufanikisha ufanisi mzuri katika utendaji. Tunaweza kusubiri siku nzima ili mtu mwingine afanye kazi kwa ajili yetu, au tunaweza kuwa sehemu ya kundi linalotafuta suluhu. Tunaweza kuwa watu wa kulalamika tu bila mwisho, au tunaweza kuchukua hatua na sisi wenyewe kuleta mabadiliko na kuwawajibisha wale wenye wajibu. Ulimwengu tunamoishi ni ule ambao tumesaidia kuumba uwe vile ulivyo au kuufanya utokee ulivyo; na ni sisi ndiyo tunaoweza kuufanya ulimwengu uwe mahali bora zaidi.

Mkurugenzi wa Twaweza, Rakesh Rajani, amesema “Fikra husafiri, tunaona jinsi wenzetu wanavyoishi na kujiletea mabadiliko, tunajiuliza ‘kama wao wanaweza, kwa nini sisi tusiweze?’, tunapata cha kujifunza, tunapata maana, tunatengeneza zana, tunajipanga, tunachukua hatua.”


--- Mwisho ---

No comments:

Post a Comment