Saturday, November 10, 2012

UAMUZI WA SPIKA KUHUSU TUHUMA KWAMBA BAADHI YA WABUNGE NA WAJUMBE WA KAMATI YA NISHATI NA MADINI.

 
 
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE LA TANZANIA
Tel: +255 22 21122065/7
Fax No. +255 22 2112538
Email:
tanzparl@parliament.go.tz
Ofisi ya Bunge
S.L.P. 941
DODOMA
____________
UAMUZI WA SPIKA
KUHUSU:
TUHUMA KWAMBA BAADHI YA WABUNGE NA WAJUMBE WA KAMATI YA NISHATI
NA MADINI WALIJIHUSISHA NA VITENDO VYA RUSHWA KATIKA KUTEKELEZA KAZI
ZAO ZA KIBUNGE
___________
Umetolewa na Mhe. Anne S. Makinda (MB.)
SPIKA
UAMUZI WA SPIKA KUHUSU TUHUMA KWAMBA BAADHI YA WABUNGE NA
WAJUMBE WA KAMATI YA NISHATI NA MADINI WALIJIHUSISHA NA VITENDO VYA
RUSHWA KATIKA KUTEKELEZA KAZI ZAO ZA KIBUNGE
[Chini ya Kanuni ya 5(1) na 72(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007,na Kifungu cha 12(1), (2)na 25(c) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296]
________________
SEHEMU YA KWANZA
Maelezo ya Utangulizi
Waheshimiwa Wabunge, mtakumbuka kwamba, tarehe 27 na 28 Julai, 2012
wakati wa mjadala waHotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, baadhi
ya Wabunge walitoa michango mbalimbali na kuibua tuhuma zilizotolewa pia
kwa maandishi, kwa barua ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw.
Eliakim C. Maswi, kwa Katibu wa Bunge kama ifuatavyo:-
Kwamba, baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Nishati na Madini walikuwa wanaenda Ofisini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini kuomba rushwa ili waitetee Wizara hiyo inapowasilisha taarifa
mbalimbali kwenye Kamati hiyo;
Kwamba, baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati hiyo wana mgongano
wa kimaslahi (conflict of interest) katika kutekeleza majukumu yao ya kibunge
ya kuisimamia Wizara ya Nishati na Madini, kwa kufanya biashara na Shirika la
Usambazi wa Umeme (TANESCO);
Kwamba, baadhi ya Wabunge wamekuwa wanajihusisha na vitendo vya
rushwa kwa kupokea fedha kutoka kwenye Makampuni ya mafuta, kwa lengo
la kuyatetea Makampuni hayo kwa kupinga uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi wa kutoa Zabuni ya Ununuzi wa
mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya IPTL kwa Kampuni ya PUMA Energy
(T) Ltd;
Kwamba, kutokana na kupewa rushwa na baadhi ya Makampuni ya mafuta ili
wayatetee, baadhi ya Wabunge walikuwa wanaendesha kampeni ya
kukwamisha kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, kwa mwaka
wa Fedha 2012/2013.
Wakati wa mjadala huo, Mheshimiwa Vita Rashid Mfaume Kawawa (MB.) alitoa
hoja kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1), 53(2) na 55(3) (f) ya Kanuni za Kudumu za
Bunge, Toleo la 2007 kwamba, kwa kuzingatia kuwamichango mingi iliyotolewa
na Wabunge wakati wa kuchangia Hotuba hiyo imewatuhumu baadhi ya
Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kujihusisha na
vitendo vya rushwa, anaomba mambo yafutayo yafanyike:-
Kamati ya Bunge na Nishati na Madini ivunjwe; na
Tuhuma za vitendo vya rushwa zilizotolewa zifanyiwe uchunguzi na Kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Baada ya Mheshimiwa Vita Rashid Mfaume Kawawa kuwasilisha hoja yake,
Bunge lilipitisha Azimio kwamba, “Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini ivunjwe; na pia kwamba, tuhuma za vitendo vya rushwa zilizotolewa
zichunguzwe na Kamati Ndogoya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na
kumshauri Spika.”
Katika kutekeleza Azimio hilo la Bunge, niliivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na
Madini, kwa kutoa tamko la kufanya hivyo Bungeni, kwa mamlaka niliyonayo
kwa mujibu wa Kanuni ya 113(3), ikisomwa pamoja na Kifungu cha 48(1) (a) cha
Sheria ya Tafsiri za Sheria, Sura ya 1 [The Interpretation of Laws Act (Cap.1)].
Aidha, kwa kuzingatia kuwa kwa hali-asili yake, jambo hilo linahusu ‘haki za
Bunge’ (Parliamentary privilege), nililipeleka kwenye Kamati Ndogo ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge ili Kamati hiyo ilifanyie uchunguzi na kunishauri.
Kamati hiyo Ndogo ilipewa Hadidu ya Rejea moja tu, ambayo ni:“Kuchunguza
na kumshauri Spika iwapo tuhuma kwabaadhi ya Wabunge na Wajumbe wa
Kamati yaNishati na Madinikujihusisha na vitendo vya rushwa ni za kweli au
hapana.”
Baada ya Kamati hiyo kukamilisha kazi yake, iliwasilisha taarifayake rasmi
kwangu ili kwa wakati muafaka,niweze kutoa Uamuzi wa Spika kuhusu suala
hilo.
Kwa kuzingatia kuwa suala hilo linahusu “haki za Bunge,” (parliamentary
privilege),napenda nitoemaelezo ya ufafanuzi kuhusu dhana hiyo kabla ya
kutoa Uamuzi wa Spika.
Dhana ya Haki za Bunge (Parliamentary Privilege) na Madhumuni yake
Kwa ajili ya Uendeshaji bora wa shughuli zake, Bunge kwa mujibu wa Katiba na
Sheria, limepewa kinga,madaraka na haki, fulani (immunities, powers and
privileges) ambazo zinaliwezesha kutekeleza majukumu yake kwa niaba ya
wananchi, kwa uhuru, uwazi na uwajibikaji, bila ya kuingiliwa au kutishwa na
mtu au chombo chochote cha Dola.
Katika Kitabu chake kiitwacho “Treaties on the Law, Privileges, Proceedings and
Usage of Parliament,1Erskine Mayametoa tafsiri ya ‘haki za Bunge’ kama
ifuatavyo:
“Parliamentary privilege is the sum of the peculiar rights enjoyed by the House
collectively… and by Members of the House individually, without which they
could not discharge their functions”2
Kwa tafsiri, nukuu hiyo inaeleza kwamba, “maana ya haki za Bunge ni haki zote
za kipekee za Bunge na za kila Mbunge binafsi kwa ujumla wake, ambazo bila
kuwepo kwake, Bunge na Wabunge hawawezi kutekeleza majukumu yao.”
Mwandishi mwingine aitwae Hood Phillips3 ameeleza kwamba, kila Bunge
linatekeleza madaraka na haki ambazo zinachukuliwa kuwa ni muhimu kwa
hadhi ya Bunge, na pia katika kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake.
Kwa ajili ya ufasaha zaidi, maelezo ya Mwandishi huyo kwa lugha aliyoitumia
yanasomeka kama ifuatavyo:-
“Each House exercises certain powers and privileges which are regarded as
essential to the dignity and proper functioning of Parliament.”
Ufafanuzi huo unaonyesha kwamba, madhumuni ya msingi ya kuwepo kwa
‘haki za Bunge’ ni kuliwezesha Bunge na Wabunge kutekeleza ipasavyo
majukumu yao ya kikatiba.
Erskine May ameelezea kuhusu madhumuni ya uwepo wa ‘haki za Bunge’ kama
ifuatavyo:-
“… certain rights and immunities such as freedom from arrest or freedom of
speech belong primarily to individual Members of the House and exist because
the House cannot perform its functions without the unimpeded use of the
services of its Members. Other such rights and immunities, such as the power to
punish for contempt and breach and the power to regulate its own constitution
belong primarily to the House as a collective body, for the protection of its
members and the vindication of its own authority and dignity. … The term
“privilege” is therefore used to mean those fundamental rights absolutely
necessary for the exercise and due execution of constitutional powers and
functions of the House.”4
Maelezo hayo yanaonyesha kwamba, uwepo wa ‘haki za Bunge’ ni nyezo
muhimu kwa ajili ya kulinda hadhi na heshima ya Bunge, na pia kwa ajili ya
kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ipasavyo. Maelezo
hayo yanaonyesha pia kwamba, haki hizo zinawalinda na kuwawezesha
Wabunge kutekeleza majukumu yao ya kibunge ndani ya Bunge na Kamati
zake, kwa uhuru, uadilifu na bila woga wa vitisho vya namna yoyoteile, kutoka
katika Mihimili ya Dola, au vyombo vingine vya Dola au watu binafsi.
Mwaka 1873, Mbunge mmoja wa Bunge la Canada alieleza kuhusu ‘haki za
Bunge’ katika maneno yafuatayo:-
“The privileges of Parliament are the privileges of the people, and the rights of
Parliament are the rights of the people.”
Kwa lugha ya Kiswahili, nukuu hiyo inaeleza kwamba, “Kinga za Bunge ni kinga
za wananchi, na haki za Bunge ni haki za wananchi.” Kwa maneno mengine,
‘haki za Bunge’ hutumiwa na Bunge na Wabunge, kwa niaba ya wananchi
wanaowawakilisha (i.e. Privileges are enjoyed by the House and by it Members
on behalf of the citizens whom they represent).
Kwa nchi yetu ya Tanzania, msingi wa ‘haki za Bunge’ letu ni Ibara ya 100 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inayoelekeza kwamba:-
“100(1) Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge
na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri
ya Muungano au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.
(2) Bila ya kuathiri Katiba hii au masharti ya Sheria nyingine yoyote, Mbunge
yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai Mahakamani kutokana na
jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au kulileta kwa njia ya
maombi, Muswada, hoja au vinginevyo,”
Kwa mujibu wa masharti ya Ibara hiyo, haki za Mbunge kikatiba ni zifuatazo:-
Kutoa mawazo yao Bungeni kwa uhuru na bila vikwazo au vitisho vyovyote;
Kutohojiwa na Mahakama au chombo chochote nje ya Bunge kutokana na
jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge;
Kutofunguliwa mashtaka ya madai au jinai kutokana na jambo au mawazo
aliyoyatoa Bungeni.
Haki na Kinga hizo zimetolewa kwa Bunge na Wabunge kwa ajili ya:
Kulinda hadhi na heshima ya Bunge kama chombo kikuuu cha Jamhuri ya
Muungano chenye madaraka kwa niaba ya wananchi, ya kuisimamia na
kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake;
na
Kuwawezesha Wabunge kutekeleza majukumu yao ya kibunge bila woga wala
kuingiliwa.
Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296[The Parliamentary
Immunities, Powers and Privileges Act (Cap.296)] imeainisha kwa ufasaha zaidi
haki za Bunge. Kifungu cha 12(2) cha Sheria hiyo kimempa madaraka Spika
kuamua kama Bunge lina mamlaka ya kusikiliza jambo lolote na kulitolea
uamuzi kama linavunja‘haki za Bunge’ (breach of privilege), na masharti ya
Kifungu hicho ndiyo yaliyozingatiwa na yanaendelea kuzingatiwa katika
kulishughulikia suala hili.
Napenda ieleweke kwamba, ‘haki za Bunge’ zinajumuisha pia haki ya
kuendesha shughuli za Bunge katika Kamati za Bunge, kwa sababu vikao vya
Kamati ni sehemu ya Bunge, na pia kwamba, Kamati za Bunge zinafanya kazi
kwa niaba ya Bunge lenyewe. Kwa kutambua hilo, Kifungu cha 5 cha Sheria ya
Kinga, Madaraka na Haki za Bunge kimetoa kinga kwa maneno yaliyosemwa
Bungeni au kwenye Kamati ya Bunge au yaliyoandikwa katika taarifa ya Bunge
au Kamati(“…words spoken before or written in a report to the Assembly or
Committee…”) ; na kwa sababu hiyo, Mbunge ana kinga ya kutoshtakiwa
kijinai, wala kwa madai, kutokana na maneno aliyoyasema au taarifa aliyoitoa
Bungeni au katika Kamati ya Bunge.
Napenda ieleweke pia kwamba, masharti ya Kifungu cha 12(1) na 13(1) vya
Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge yanaelekeza kwamba, katika
kutilia nguvu uhuru na haki zake, Bunge kwa kuzingatia Katiba na Kanuni za
Bunge, lina madaraka ya kufanya yafuatayo:-
Kusikiliza na kuamua kuhusu mambo yote yanayovunja ‘haki za Bunge’
(contempt or breach of privilege) ndani ya Bunge, isipokuwa makosa ya kijinai.
Kuita na kuhoji mashahidi kwa ajili ya kuthibitisha jambo lolote linalohitaji
kuamuliwa na Bunge au Kamati ya Bunge.
Kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha 12(2) cha Sheria hiyo, Uamuzi wa kama
jambo fulani linavunja‘haki za Bunge’ au la, unapaswa ufanywe na Spika, kwa
kuzingatia utaratibu uliowekwa na Kanuni za Bunge.
Kutokana na madaraka aliyonayo kwa mujibu wa Kifungu cha 12(1) na (2) cha
Sheria hiyo, Spika ana wajibu wa kulinda na kutetea ‘haki za Bunge’ kwa
sababu, bilaya kuwa na ‘haki’ hizo za msingi ambazo ni uhuru wa mawazo,
majadiliano na utaratibu, ni dhahiri kwamba Bunge na Wabunge watashindwa
kutekeleza majukumu yao ya kikatiba, na pia watashindwa kutekeleza wajibu
wao kwa wapiga kura na wananchi wanaowawakilisha kwa ujumla. Kama
ilivyo kwa umuhimu kwa Mahakama, wa kuwepo kwa‘uhuru wa Mahakama’
katika kutekeleza jukumu lake la utoaji haki, ‘haki za Bunge’ zina umuhimu
katika utekelezaji wa majukumu ya kikatiba ya Bunge, na kwa sababu hiyo,‘haki
za Bunge’ zinapaswa kulindwa na Bunge lenyewe, kupitia kwa Spika.
Aidha, Vifunguvya 12(1)-(4) vya Sheria hiyo vimetamka bayana kwamba,
mambo yanayohusu ‘hakiza Bunge’ yasiyo ya kijinai, yanaweza kutiliwa nguvu
na Bunge lenyewe ndaniya Bunge, na yale ambayo ni ya kijinai, yanapaswa
kushughulikiwa na Mahakama.
Waheshimiwa Wabunge, baada ya kutoa maelezo haya ya ufafanuzi
kuhusudhana ya ‘haki za Bunge’, napenda sasa nirejee kwenye suala lenyewe
ambalo ndio msingi wa Uamuzi nitakaoutoa.
Msingi wa Suala Husika
Kama nilivyoeleza kwenye maelezo yangu ya utangulizi, msingi wa suala hili
linalohusu‘haki za Bunge’,ni “tuhuma kwamba, baadhi ya Wabunge na
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini walijihusisha na vitendo vya
rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge.”
Waheshimiwa Wabunge, ni dhahiri kwamba, tuhuma kuwa baadhi ya
Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini
wanajihusisha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya
kibunge, ni suala linalohusu uvunjaji wa ‘haki za Bunge’ (breach of
parliamentary privilege).
Hakuna ubishi kwamba, kitendo cha Mbunge kuomba au kupokea rushwa kwa
madhumuni ya kutumia wadhifa wake kama Mbunge kutekeleza matakwa
fulani ya Kampuni, Shirika au ya mtu yeyote binafsi, ni uvunjaji mkubwa wa ‘haki
za Bunge’ (a serious breach of parliamentary privilege), na pia
iwapokimethibitika pasipo mashaka yoyote, ni kosa la jinai.
Kuhusiana na hilo, Erskine May ameeleza kwamba:-
“The acceptance by a Member… of a bribe to influence him in his conduct as a
Member, or of any fee, compensation or reward in connection with the
promotion of or opposition to any bill, resolution, matter or thing submitted or
intended to be submitted to the House, or to a Committee, is contempt.”
Tafsiri ya maelezo hayo ni kwamba, “upokeaji wa rushwa kwa Mbunge kama
kishawishi cha kumfanya atende kazi zake za kibunge, au kama malipo, fidia au
zawadi kwa ajili ya kuunga mkono aukutounga mkono Muswada wa Sheria,
Azimio, au jambo lingine lolote lililowasilishwa au linalokusudiwa kuwasilishwa
Bungeni, au kwenye Kamati ya Bunge, ni kitendo cha kulidhalilisha na
kulifedhehesha Bunge.”
Hali kadhalika, kitendo cha Mbunge kuomba au kupokea rushwa kwa
madhumuni ya kutumia wadhifawake kama Mbunge kutekeleza matakwa au
maslahi fulani ya Kampuni, Shirika au ya mtu yeyotebinafsi, kama kimethibitika
pasipo mashaka yoyote, ni kosa la jinai, kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha
28(1), (2) na 32 cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296.
Vifungu hivyo vinasomeka kama ifuatavyo:-
“28(1) Any person who offers to any Member or officer… either directly or
indirectly any bribe, fee, compensation, gift or reward in order to influence such
member or officer in his conduct as such member or officer or for or in respect of
the promotion of or opposition to any Bill, resolution, matter, rule or thing
submitted to or intended to be submitted to the Assembly shall be guilty of an
offence.
(2) Any member or officer… who demands, accepts or receives directly or
indirectly, any bribe, fee, compensation, gift or reward, the offering of which is
or would be an offence under this section, shall be guilty of an offence.”
“32. any member who accepts or agrees to accept or obtains or attempts to
obtain for himself or for any other person any bribe, fee, compensation, reward
or benefit of any kind for speaking, voting or acting as such member or for
refraining from so speaking, voting or acting on account of his having so spoken,
voted or acted or having so refrained, shall be guilty of an offence…”
Hoja ya Kutolewa Uamuzi
Waheshimiwa Wabunge, hoja ambayo natakiwa niitolee Uamuzi kuhusiana na
suala hili ni moja tu, nayoni je, kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi
uliofanywa na Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, tuhuma
za baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini
kujihusisha na vitendo vya rushwa zimethibitishwa au hapana.?
Kwa mazingira ya suala hili, nimeona kuna ulazima wa kueleza matokeo ya
uchunguzi wa Kamati hiyo kwa kila tuhuma, kwa ajili ya kuondoa mashaka
yoyote kwa Uamuzi nitakaoutoa.
SEHEMU YA PILI
Matokeo ya Uchunguzi wa Kamati
Waheshimiwa Wabunge, tuhuma mahsusi zinazohusu baadhi ya Wabunge na
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya
rushwa katika utekelezaji wa majukumu yaoya kibunge zilizochunguzwa na
Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ni zifuatazo:-
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi, kwa mujibu
wa barua yake kwa Katibu wa Bunge Kumb. Na. SAB.88/223/01/28 ya tarehe 31
Julai, 1012 alimtuhumu Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.) kwamba tarehe 6 Februari,
2012, Mheshimiwa huyo alikwenda ofisini kwa Katibu Mkuu huyo wa Wizara, mjini
Dodoma, ambapo alimwomba ampe rushwa ya Shilingi milioni hamsini (sh.
50,000,000/=) kwa ajili ya kuwagawia baadhi ya Wabunge na baadhi ya
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, ili watetee mipango
ambayo Wizara ya Nishati na Madini itakuwa inaiwasilisha kwenye Kamati ya
Bunge ya Nishati na Madini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi, kwa barua
hiyo hiyo alidaikwamba, tarehe 4 Juni, 2012, Mhe. Selemani Jumanne Zedi (MB.)
alimtaka Bw. Eliakim C. Maswi awalipe Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati
na Madini, Shilingi milioni mbili (sh. 2,000,000/=) kwa kila Mjumbe, ili
awatulizeau‘awazibe midomo’ wasiendelee kumshambulia yeye (Bw. Eliakim C.
Maswi) kutokana na utendaji wake waliokuwa wanaulalamikia.
Katika michango mbalimbali iliyotolewa Bungeni wakati wakujadili Bajeti ya
Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa Fedha 2012/2013, Wabunge
kadhaa walituhumu baadhi ya Wabunge na pia Wajumbe wa Kamati ya
Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa
majukumu yao ya kibunge, kwa kupewa rushwa na Makampuni ya mafuta ili
wayatetee kuhusiana na Zabuni ya Ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea
mitambo ya IPTL.
Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter Muhongo (MB.) kuwatuhumu
baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa na
mgongano wa kimaslahi kwa kufanya biashara na Shirika la Kusambaza
Umeme (TANESCO).
Matokeo ya uchunguzi wa Kamati kwa kila moja ya tuhuma zilizoainishwa hapo
juu, kwa mujibu wa Taarifa ya uchunguzi iliyowasilishwa na Kamati kwa
kuzingatia Hadidu za Rejea iliyopewa, ni kama ifuatavyo:-
Tuhuma dhidi ya Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.), ya kwamba alimwomba Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi, rushwa ya Shilingi
milioni hamsini (sh. 50,000,000/=)
Kuhusiana na tuhuma hiyo, uchunguzi wa Kamati ulibaini yafuatayo:-
Kwamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. EliakimC. Maswi
aliibua tuhuma hiyo kama njia ya kujihami dhidi ya tishio la Wabunge Mhe.
Munde Tambwe Abdallah, Mhe. Sara Msafiri Ally na Mhe. Christopher Ole-
Sendeka ambao, kwa ushahidi wake wa maandishi, Bw. Eliakim C. Maswi
ameeleza kwamba, walitamka ni lazima aachie nafasi yake ya Ukatibu Mkuu,
kwa kuwajibika kutokana na utendaji wake usioridhisha.
Katika kutoa ushahidi wake alipoulizwa na Kamati kwamba, “… Mheshimiwa
Sara asingekuambia uachie Ukatibu Mkuu usingemtuhumu kwamba alikuja
kukuomba rushwa, ila ulilazimika kuzua tuhuma hizo baada ya kuona nafasi
yako inatishiwa…”, Bw. Eliakimu C. Maswi alijibu kama ifuatavyo:
“Nakubali alitamka hivyo mbele ya Waziri Mkuu kwamba, mimi sina sababu za
kuendelea kuwa Katibu Mkuu, sasa na mimi mtu akiniambia hivyo, na yeye
kwanini aendelee kuwa Mbunge?”
Kwamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi
ambaye, kwamujibuwa barua yake kwa Katibu wa Bunge Kumb. Na.
SAB.88/223/01/28 ya tarehe 31 Julai, 2012 ndiye alitoa tuhuma hii na ndiye
aliyekuwa na jukumu la kuthibitisha, ameshindwa kuthibitisha ukweli wa tuhuma
yake.
Kwamba, ukweli wa tuhuma kuwa Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.) aliomba rushwa
ya Shilingi milioni hamsini kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Bw. Eliakim C. Maswi haukuthibitika. Kilichothibitika ni kwamba, Katibu
Mkuu huyo alizua tuhuma hii kwa nia ya kujihami dhidi ya baadhi ya Wajumbe
wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini waliokuwa wanahoji kuhusu utendaji
wa Wizara yake, hususan ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma katika
ununuzi wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL, na
utekelezaji wa mpango wa upatikanaji wa umeme wa dharura.
Tuhuma dhidi ya Mhe. Selemani Jumanne Zedi (MB.), kwamba alimwomba
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi, rushwaya
Shilingi milioni mbili (sh. 2,000,000/=) kwa kila Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya
Nishati na Madini.
Kuhusu tuhuma hii, uchunguzi wa Kamati ulibaini yafuatayo:-
Kwamba,matamshi ya baadhi ya Wajumbe wa Kamatiya Bunge ya Nishati na
Madini ambao ni,Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.), Mhe. Munde Abdallah Tambwe
(MB.), Mhe. Christopher ole-Sendeka (MB.) na Mhe. Selemani Jumanne Zedi
(MB.) kwamba, ni lazima Bw. Eliakim C. Maswi aachie nafasi kwa sababu
hastahili kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,yalimfanya Katibu
Mkuu huyo atafute mbinu ya kujihami dhidi ya tishio hilo.
Mbinu aliyoitumia, ni kutaka kuwalipa fedha Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya
Nishati na Madini, shilingi milioni mbili (sh.2,000,000/=) kwa kila Mjumbe, kwa
sharti la kuwataka wamsainie nyaraka za kukiri kupokea fedha hizo, lakini mbinu
hiyo haikufanikiwa, na mbinu hiyo iliposhindikana, aliamua kuzua tuhuma za
rushwa dhidi ya Wabunge hao.
Kwamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi
ndiye alitaka kuwalipa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini,
kwalengo la ‘kuwafunga midomo’wasiendelee na madai yao ya kumtaka
awajibike kwa kuachia nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Wizara,kuhusiana na suala la
utekelezaji usioridhisha wa Mpango wa uzalishaji wa umeme wa dharura (bilioni
408) na kuhusiana na ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya
IPTLkutozingatia Sheria.
Tuhuma Zilizotolewa na Wabunge Wakati wa kujadili Bajeti ya Wizara ya Nishati
na Madini kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013, kwamba baadhi ya Wabunge na
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wanajihusisha na vitendo
vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge, kwa kupewa
rushwa na Makampuni ya Mafutaili wayatetee kuhusiana na Zabuni yaUnunuzi
wa Mafuta Mazito ya Kuendeshea Mitambo ya IPTL.
5.2.3.1 Katika Uchunguzi wake kuhusu tuhuma hii, Kamati ilibaini yafuatayo:-
Kwamba,katika Wizara ya Nishati na Madini kulifanyika ununuzi wa dharura wa
mafuta mazito kiasi cha zaidi ya lita milioni kumi, kutoka katika Kampuni ya
PUMA Energy (T) Ltd., kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya IPTL. Ununuzi huo
ulifanyika wakati tayari Shirika la kusambaza Umeme (TANESCO) lilishaingia
Mikataba na Kampuninyingine kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya aina hiyo, na
kwa lengo lile lile la kuendeshea mitambo ya IPTL, hali ambayo ilizua shaka kwa
Mhe. Christopher Ole-Sendeka (MB.) ambaye, kwa kuamini kwamba utaratibu
wa Ununuzi wa mafuta hayo uliofanywa na Wizara ulikuwa umekiuka Sheria ya
Ununzuzi wa Umma, Namba 7 ya Mwaka 2011, alianza kuwashawishi (lobbying)
Wabunge kadhaa iliwaunge mkonohoja yake aliyokusudia kuiwasilisha kwa ajili
ya kuitaka Serikali itoe maelezo kuondoa shaka hiyo ya ukiukwaji wa Sheria.
Kwamba, kutokana na Mhe. Christopher Ole-Sendeka (MB.) kushikilia msimamo
wa kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, pamoja na
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Eliakim C. Maswi
na baadhi ya Wabunge ambao ni Mhe. Joseph R. Selasini, Mhe. Ally Kessy
Mohamed, Mhe. Vick Kamata na Mhe. Alphaxard Kangi Lugola walianza kutilia
shaka msimamo huo wakidhani kwamba, Mhe. Christopher Ole-Sendeka
alikuwa amepewa rushwa na Makampuni ya Mafuta.
Kwamba, tuhuma hii kuwa baadhi ya Wabunge na Wajumbe wa Kamati ya
Bunge ya Nishati na Madini walikuwa wamepewa rushwa na Makampuniya
Mafuta ili waibane Wizaraya Nishati na Madini kuhusu Ununuzi wa mafuta ya
kuendeshea mitambo ya IPTL kufanywa kinyume cha utaratibu uliowekwa na
Sheria ya Ununuzi wa Umma, haikuweza kuthibitika kama inavyoonyeshwa na
majibu ya Wabunge walioitoa tuhuma hiyo Bungeni, walipotakiwa watoe
ushahidi kuthibitisha ukweli wake:
Mhe. Joseph R. Selasini (MB.)
Mhe. Joseph R. Selasini (MB.) alitamka Bungeni kwamba:
“Makampuni ya Mafuta yalikuwa hapa Dodoma yakigawa fedha. Ni lazima
niseme kuna wenzetu wanasema kwa sauti kubwa, kuna wenzetu wanasema
kwa mbwembe, lakini sasa naamini wanasema kwa nguvu ya chochote kilicho
mfukoni…” .
Alipotakiwa na Kamati kuthibitisha ukweli wa tuhuma hiyo, majibu ya Mhe.
Joseph R. Selasini (MB.) yalikuwa kama ifuatavyo:-
“… Kabla ya Hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini haijasomwa Bungeni,
kulikuwa na mino-ng’ono mingi sana, kwamba baadhi ya Wabunge na baadhi
ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini walikuwa wamepewa
fedha ili kutoa ushawishi wa kukwamisha Bajeti hiyo na kushinikiza Waziri na
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo wawajibike kwa kuachia nyadhifa zao. … Lazima
niwe wazi, majina ya Wabunge hao yalikuwa yanatajwa, Mhe. Christopher Ole-
Sendeka, Mhe. Anne Kilango, Mhe. Zedi, Mhe. Lembeli, Mhe. Tambwe, Mhe.
Sara Msafiri na Mhe. Zitto Kabwe, ingawaje binafsi sina ushahidi kama kweli
walichukua fedha au hawa-kuchukua.
Kwa kutambua kwamba rushwa ni kitu kibaya, na nikiwa Mbunge napaswa
kusimamia ‘public interest’, niliamua kuzungumza ili mjadala mpana ufanyike na
kama yeyote ana ushahidi utolewe… kwa ajili ya kunusuru hadhi na heshima ya
Bunge letu.”
Swali: “Kwa hiyo , huna ushahidi wowote kuhusu Mbunge nani kapewa rushwa,
nani kapokea rushwa, zilikuwa tuhuma tu?”
Jibu: “… Mimi sina ushahidi wa moja kwa moja kwamba fulani kapokea na
kapokea kiasi gani. Kama nilivyosema, Wabunge katika ujumla wao walikuwa
wanatuhumu na sijui kama walikuwa na ushahidi au hawana.”
Mhe. John John Mnyika (MB.)
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Nishati na Madini,
Mhe John John Mnyika (MB.) wakati akiwasilisha Maoni ya Kambi hiyo Bungeni
alitamka kama ifuatavyo:-
“… Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba kuna kampeni
kubwa inafanywa ndani na nje ya Bunge ili Uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati, Bw. Eliakim C. Maswi ubatilishwe kwa maslahi ya Makampuni
yaliyokosa Zabuni ya kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendesha mitambo ya kufua
umeme ya IPTL na Wapambe wake wa ndani na nje ya Bunge. Aidha,
wanaoendesha kampeni hiyo wanashinikiza Katibu Mkuu huyo ajiuzulu kwa kile
kinachoitwa kitendo chake cha kukiuka Sheria ya Ununuzi wa Umma.”
Alipotakiwa na Kamati kuthibitisha ukweli wa tuhuma hiyo, Mhe. John John
Mnyika (MB.) alitoa maelezo yafuatayo:-
“…Vyombo mbalimbali vya Habari vimeandika kwa mfululizo, habari
zinazoeleza tuhuma ya masuala ya ununuzi wa mafuta. Baadhi ya habari hizo
zimenukuu Wabunge kwa majina yao… na mpaka naingia kusoma Hotuba
Bungeni tarehe 27 Julai, hakukuwahi kuwa na kanusho la habari hizo.”
Mhe. Alphaxard Kangi Lugola (MB.)
Mhe. Alphaxard Kangi Lugola (MB.) alipotakiwa na Kamati kuthibitisha ukweli
wa tuhuma alizozisema Bungeni kwamba “… kuna watu wameanza kutumia
Bunge kwa kudhani Wabunge tunakimbilia peremende na vipesa vyao ili
kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza matakwa yao, na kwamba Nchi
haitawaliki kwa kukosa umeme,” maelezo yake yalikuwa kama ifuatavyo:-
“… nilisema maneno hayo kutokana na uzalendo nilionao na kwa uchungu
nilionao. Nilichangia Bungeni ili tu ku-pre-empty kama wapo watu waliojiandaa
kuwahonga Wabunge wajue kwamba sisi Wabunge hatuko tayari kutumika.”
Mhe. Ally Keissy Mohamed (MB.)
Katika kutaka kupata ushahidi kuhusiana na tuhuma hii ya rushwa, mahojiano
ya Kamati na Mhe. Ally Keissy Mohamed (MB.) yalikuwa kama ifuatavyo:-
Swali: “Mbali na hisia zako tu kwamba Wabunge hawa waliokuwa
wanampinga Waziri, wanampinga Katibu Mkuu, kwamba lazima wamepewa
chochote, je, una ushahidi mwingine zaidi ya huo?”
Jibu: “Huu ni ushahidi wa kukisia, mtu yeyote mwenye akili timamu lazima atajua
kuna chochote.”
Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter M. Muhongo (MB.)
Mahojiano kati ya Kamati na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter M.
Muhongo (MB.) yalikuwa kama ifuatavyo:-
Swali: “Unaithibitishiaje Kamati hii kwamba madai hayo ya Makampuni ya
mafuta kuwepo Dodoma na kugawa fedha kwa Wabunge?”
Jibu: “Mhe. Mwenyekiti, nadhani naomba nikukumbushe kwamba, mambo
yote ambayo mtakuwa mnayasikia kutoka kwangu na kutoka kwa wengine
ambao mnahitaji kuwahoji yatakuwa ni ‘allegations’,..”
Nukuu za Mahojiano hapo juu kati ya Kamati na mashahidi waliohojiwa
zinaonyesha wazi kwamba, hakuna ushahidi wowote uliotolewa kama
uthibitisho wa tuhuma hii ya Makampuni ya mafuta kuwapa rushwa Wabunge.
Tuhuma Iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter M. Muhongo
(MB.), kwamba baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini
wana Mgongano wa kimaslahi (Conflict of Interest) kwa Kufanya Biashara na
TANESCO
Tuhuma hii ilitolewa na Waziri wa Nishati na Madini, . Prof. Sospeter M. Muhongo
(MB.) alipokuwa akihitimisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara yake Bungeni, kama
ifuatavyo:-
“… tunao ushahidi usio na shaka wa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge na
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kufanya
biashara na TANESCO… baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameingia
Mkataba wa kuiuzia TANESCO matairi na kushinikiza kubadili bei ya matairi hayo
baada ya mkataba kufungwa…”
Tuhuma hii pia ilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw.
Eliakim C. Maswi katika barua aliyomwandikia Katibu wa Bunge, akitaja
kwamba, Mhe. Sara Msafiri Ally(MB.),pamoja na Mhe. Munde Tambwe
Abdallah(MB.) wanafanya biashara yamatairina TANESCO.
Aidha, tuhuma hii ilitolewa pia na Mhe. Tundu A. M. Lissu (MB.), katika Mkutano
na Waandishi wa Habari kwa kumtaja Mhe. Sara MsafiriAlly(MB.) na Mhe.
Munde Tambwe Abdallah (MB.) kwamba, kwa taarifa alizonazo Wabunge hao
walikuwa na mgongano wa kimaslahi katika utekelezaji wa majukumu yao ya
kibunge, kwakuwa wanafanya biashara na TANESCO wakati wao ni Wajumbe
wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, yenye jukumu la kuisimamia Wizara
ya Nishati na Madini.
Katika Uchunguzi wa kupata ukweli kuhusu tuhuma hii, Kamati ilichambua
nyaraka zilizowasilishwa kama vielelezo, pamoja na maelezo ya mashahidi
waliohojiwa, ambapo Kamati ilibaini yafuatayo:-
Kampuni iliyoingia Mkataba na TANESCO kwa ajiliya kuiuzia TANESCO matairi
inaitwa “Shariffs Services and General Supply Limited,” ambayo kwa mujibu wa
taarifa za Mamlaka ya Usajiri wa Makampuni (BRELA), Mhe. Sara Msafiri Ally
(MB.) na Mhe. Munde Tambwe Abdallah (MB.) siyo wamiliki wala wanahisa wa
Kampuni hiyo.
Hakuna mahali popote katika hatua za mchakato wa Zabuni ya Kuiuzia
TANESCO matairi ambapo Wabunge waliotuhumiwa wamehusika.
Kitendo cha Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.) kufuatilia kusainiwa kwa Mkataba
ambao TANESCO ilikuwa imeupitisha, kuchukua nakala na kumpelekea Mhusika
ambaye ni jirani yake, siuthibitisho wa kutosha kwamba, Mhe. Sara Msafiri
Ally(MB.) ndiye anayefanya biashara ya kuiuzia matairi TANESCO, au kuwa yeye
ndiye mmiliki wa Kampuni iliyoingia Mkataba wa kuiuzia matairi TANESCO.
Ukweli wa kauli iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter
M. Muhongo (MB.) Bungeni, “kwamba baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya
Bunge ya Nishati na Madini wana mgongano wa kimaslahi katika utekelezaji wa
majukumu yao ya kibunge kwa kufanya biashara ya kuiuzia matairi TANESCO”
haukuthibitishwa.
Madai ya Mhe. Tundu A. M. Lisu (MB.) kuhusu Mhe. Sara Msafiri Ally (MB.) na
Mhe. Munde Tambwe Abdallah (MB.) kuwa na mgongano wa kimaslahi
hayana ukweli pia, kwa sababu alipotakiwa na Kamati kuthibitisha ukweli
kuhusu madai hayo, maelezo yake yalikuwa kama ifuatavyo:
“… ni kweli nilifanya huo Mkutano na Waandishi wa Habari, na ni kweli vilevile
kwamba, nilitaja majina ya Mhe. Sara Msafiri na Mhe. Munde Tambwe kama
Wabunge ambao nilisema wana matatizo ya mgongano wa kimaslahi kama
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Niseme kifupi niliyatoa wapi hayo maneno. Siku moja au mbili kabla ya Bajeti
yaWizara ya Nishati na Madini kuwasilishwa Bungeni, nilifanya vikao kadhaa na
Waziri mwenyewe Mhe. Prof. Muhongo, Naibu Waziri Mhe. Dkt. Masele na Katibu
Mkuu, Bw. Maswi, katika Ofisi za Wizara hapa Dodoma, kwa ajili ya kufuatilia
matatizo ya TANESCO na huo mgogoro wa tuhuma dhidi ya TANESCO.
Kwahiyo, niliyoyasema siku ya ‘Press Conference’ yalitokana na taarifa ambayo
niliipata kutoka kwa hao Waheshimiwa niliowataja.”
Habari za kuambiwa (hear say) haziwezi kuchukuliwa kama ni ushahidi wa
kuthibitisha madai au tukio fulani.
Ukweli wa tuhuma, kwamba baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya
Nishati na Madini wanafanya biashara ya kuiuzia TANESCO matairi ya magari
na walihusika kutaka kubadilisha bei ya matairi hayo baada ya Mkataba
kufungwa, haukuthibitika pia.
SEHEMU YA TATU
MAELEKEZO YA SPIKA
Waheshimiwa Wabunge, napenda kumshukuru kwa dhati Mhe. Brig. Jenerali
(Mst.) Hassan A. Ngwilizi (MB.), Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge, pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati hiyo,
kwa umakini wao katika kuchunguza tuhuma zinazohusika, na kuwasilisha
taarifa yao ya Uchunguzi na Ushauri kwangu.
Waheshimiwa Wabunge,tuhuma ya Wabunge kujihusisha na vitendo vya
rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge ni nzito na haiwezi
kupuuzwa hata kidogo. Kwa kuzingatia uzito wa tuhuma yenyewe, ndiyo
maana niliivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini baada ya Bunge
kupitishaAzimio la kufanya hivyo, na kuagiza tuhuma hiyo ifanyiwe uchunguzi ili
kubaini ukweli wake.
Kupokea rushwa ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria za nchi, na kwa vitendo
vya jinai, Mbunge yeyote hana kinga, na kama nilivyoeleza hapo awali, Sheria
ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296 imeweka bayana mambo
yanayohusu haki za Bunge yanayoweza kutiliwa nguvu na Bunge lenyewe
ndani ya Bunge, na yale ambayo yanapaswa kushughulikiwa na Mahakama.
Tuhuma hii ni kati ya mambo ambayo yana sura mbili kwa pamoja, yaani ni
kosa la kijinai, na ni jambo linalopaswa kushughulikiwa na Bunge lenyewe, ndani
ya Bunge, kutokana na kuwa ni jambo linalohusu haki za Bunge.
Iwapo matokeoya uchunguzi wa Kamati yangeonyesha kuwepo kwa ushahidi
kwamba tuhuma husikazimethibitishwa, ningepaswa kuwasiliana na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuchukua
hatua zinazohusika, kwa mujibu wa Kifungu cha 12(4) cha Sheria ya Kinga,
Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296.
Suala hili limetupa somo na mfano mzuri wa mazoea yasiyofaa ya Wabunge wa
Bunge hili kusema jambo lolote Bungeni bila kufanya utafiti wa kutosha wa
kupata ukweli wa jambo lenyewe au taarifakuhusu hilo analolisema, na hasa
kama linahusu tuhuma kwa taasisi au mtu binafsi;na kwa sababu hiyo, kuna
umuhimu waWabunge kujizuia kusema mambo ambayo ni tetesi tu (rumours),
na pia ni lazimaWabunge wajizuie na tabia yakutaka kusema tu kuhusu jambo
lolote ili wasikike, bila ya kuwa na ukweli wa jambo lenyewe.
Aidha, kwa mambo ya kibunge ambayo yamewekewautaratibu na Kanuni za
Bunge, ni vizuri Wabunge wayatekeleze kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa
na Kanuni hizo za Bunge. Kwa mfano, kama Mbunge anahisiwa kuwa na tatizo
la mgongano wa kimaslahi, Kanuni za Bunge zinaelekeza nini kifanyike. Mazoea
ya kwenda kuvitangazia vyombo vya habari kuhusu suala kama hilo ni kinyume
cha utaratibu uliowekwa na Kanuni za Bunge.
Waheshimiwa Wabunge, lazima niseme wazi kwamba, vitendo vyovyote
vinavyovunja ‘hakiza Bunge’na pia kuathiri hadhi na heshima ya Bunge, kama
vile rushwa n.k. havitavumiliwa na Bunge hata kidogo. Vitendo kama hivyo
vitakemewa na kuchukuliwa hatua zinazostahili mara
vitakapothibitika.Sambamba na hilo, vitendo vya kulizushia Bunge tuhuma za
uongo na kulizuia Bunge au Kamati yoyoteya Bunge kutekeleza ipasavyo
majukumu yake, havitavumiliwa hata kidogo, kwa sababu ni hatari kwa
mustakabali wa Taifa letu.
Vitendo kama hivyo vya kuzusha tuhuma za kutunga zisizo na ukweli dhidi ya
Bunge, si kwamba tu,vinalifedhehesha na kulidhalilisha Bunge, bali pia vinalizuia
Bunge kutekeleza majukumu yake ya kikatiba, na vilevile vinawawekea kikwazo
Wabunge wasitimize wajibu wao kwa Bunge, kwa wapiga kura wao, kwa
wananchi kwa ujumla na pia kwa Taifa.
Kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu ya Bunge, hususani
kuisimamia na kuishauri Serikali kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 63(2) ya
Katiba, utendaji wa Kamati za Bunge hautakiwi uwe ni wa‘kuingilia majukumu
ya kiutendaji ya Serikali, kwa sababu kwa kufanya hivyo, Kamati za Bunge na
zenyewe zinakuwa ni sehemu ya Serikali ambayo zinatakiwa ziisimamie na
kuishauri. Kwa kuzingatia udhaifu uliojitokeza katika eneo hilo, kuanzia sasa,
suala hili litafuatiliwa na kuratibiwa kwa karibu ili kuhakikisha kwamba kuna
utekelezaji bora wa majukumu ya kikatiba ya Bunge.
Aidha, ni muhimu kwa nidhamu na mienendo (conduct) ya Wabunge kuwa
katika kiwango (standard)cha Mbunge ambaye anatazamwa na jamii kama ni
Kiongozi na mfano mzuri wa kuigwa.Haitakiwi mwenendo na Maadili ya
Kiongozi kama Mbunge kuwa na dosari au kutiliwa mashaka kutokana na
matendo maovu yasiyotegemewa kufanywa na Kiogozi wa Umma.Ili kusimamia
ipasavyo nidhamu za Wabunge, Kanuni za Maadili (Code of Conduct) kwa
Wabunge zimeandaliwa na zinategemewa kupitishwa hivi karibuni, ambapo
masuala ya nidhamu kwa Wabunge yataratibiwa na kuchukuliwa hatua
zinazostahili, kwa ajili ya kulinda hadhi na heshimaya Bunge na Wabunge.
Kwa kuzingatia kuwa matokeo ya uchunguzi wa Kamati yameonyesha kwamba
tuhuma husikahazikuweza kuthibitishwa; na kwakuwa uzito wa tuhuma zenyewe
umeathiri kwa kiasi kikubwa, hadhi na heshima ya Bunge kama Taasisi, na pia
hadhi na heshima ya Wabunge waliohusishwa; na kwakuwa, kwa mujibu wa
masharti ya Kifungu cha 25(c) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za
Bunge, Sura ya 296, suala husika linahusu ‘haki za Bunge’, na linapaswa
kutolewa Uamuzi na Spika kwa mujibu wa utaratibu wa kibunge; sasanatoa
Uamuzi wa Spika kama ifuatavyo:-
UAMUZI WA SPIKA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi
amelifedhehesha na kulidhalilisha Bunge kwa kuzusha tuhuma za Uongo na
kuufanya Umma wa Watanzania kuamini kwamba, baadhi ya Wabunge na
Wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini wanajihusisha na vitendo vya rushwa;
na kwa kufanya hivyo ametenda kosa la kuvunja haki za Bunge, na anastahili
adhabu.
Kwakuwa, baada ya kosa hilo kufanywa, uwepo wa uhusiano mzuri kati ya
Bunge na Serikali kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla, ni jambo
linalopaswa kupewa umuhimu wa kwanza,Uamuzi wa Spika ni kwamba, natoa
onyo kali kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C.
Maswi, na kumtaka asirudie tena kosa hilo la kuzua tuhuma za uongo dhidi ya
Bunge na Wabunge.
(a) Wabunge Walioisemea Tuhuma Bungeni
Kwakuwa, Wabunge waliolisema suala hili la rushwa Bungeni, walilisemea kwa
nia njema ya kulikemea, na hawakumtaja Mbunge yeyote kuhusika nalo; na
kwakuwa pamoja na nia hiyo njema Wabunge hao walilisemea suala hilo bila
ya kufanya utafiti kupata ukweli wake, Uamuzi wa Spika ni kwamba, Wabunge
hao nawapa onyo kali na kuwataka wasirudie kosa hilo la kuzungumzia jambo
Bungeni wasilokuwa na uhakika nalo.
(c) Mhe. Tundu A. M. Lissu (MB.)
Kwakuwa Mhe. Tundu A. M. Lissu (MB.) alikuwa na fursa ya kulisemea suala ya
mgongano wa maslahi kwa Wabunge wahusika Bungeni, lakini aliamua
kulisemea nje ya Bunge, kwa kutoa tuhuma dhidi ya Wabunge kuhusiana na
suala hilo kwenye Vyombo vya habari, kwa kuwataja majina, kwa ushahidi wa
‘habari za kuambiwa’ (hear say), kinyume na masharti ya Kanuni ya 61(2) ya
Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007; na kwakuwa kwa kufanya hivyo
aliwadhalilisha na kuwafedhehesha Wabunge hao; Uamuzi wa Spika ni
kwamba, nampa onyo kali Mhe. Tundu A. M. Lissu, na kumtaka asirudie kosa hilo
la kuvunja Kanuni za Bunge, na pia kuzungumzia jambo bila ya kuwa na
uhakika nalo. Pamoja na onyo hilo, wale Wabunge waliotajwa na Mhe. Tundu
Lissu nawaomba wamsamehe ili tuanze ukurasa mpya wa kupendana,
kuheshimiana na kuvumiliana.
(d) Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter M. Muhongo (MB.)
Kwakuwa, kauli ya Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter Muhongo
(MB.) kwamba, “upo ushahidi usio na mashaka kwamba wapo baadhi ya
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wanaofanya biashara ya
kuiuzia matairi TANESCO, na kwamba kwa kufanya hivyo, wana mgongano wa
kimaslahi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge ya kuisimamia
Serikali” aliitoa Bungeni, ambapo ukweli wake haukuweza kuthibitishwa, Uamuzi
wa Spika ni kwamba, Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Prof. Sospeter M.
Muhongo (MB.) anatakiwa awe mwangalifu anapotoa kauli Bungeni, kwa
sababu kauli za Mawaziri huchukuliwa kuwa ni kauli za Serikali. Hivyo anapotoa
kauli yoyote Bungeni, ahakikishe kuwa ana uhakika wa ukweli wa jambo
analolisema
Uamuzi huu nimeutoa Bungeni, Dodoma leo tarehe 9 Novemba, 2012.
Anne S. Makinda (MB.)
SPIKA WA BUNGE

No comments:

Post a Comment