Monday, November 26, 2012

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete alimwapisha Jaji Bethuel Mmila kuwa jaji wa Mahakama ya Rufaa

Sunday, November 25, 2012

MLEMAVU WA NGOZI MARIAMU STANFORD AKIWA NA CHETI CHAKE BAADA YA KUHITIMU KWENYE MAHAFALI MJINI MOSHI

Mariam Stanford mlemavu wa ngozi ambaye mikono yake ilikatwa na watu mwaka 2008 akiwa ameshika cheti chake baada ya kuhitimu katika Chuo cha Ufundi cha Imani Vocational Training Centre kilichpo Moshi, Kilimanjaro.Picha kwa hisani ya  UTSS)



WAISLAM WA MADHEHEBU YA SHIA ITHNA ASHER WAADHIMISHA SIKUKUU YA ASHURA IKIWA NI KUMBUKUMBU YA KUUAWA KWA MJUKUU WA MTUME MUHAMMAD,IMAMU HUSSEIN (AS) JIJINI DAR ES SAALAM


Saturday, November 24, 2012

MAFUNZO YA MUZIKI

Mwalimu wa nadharia na Gitaa Abeid Mussa akiwaelekeza wanafunzi namna ya kupangilia muziki wakati wa kufanya onyesho

Mahojiano ya moja kwa moja na Mhe. Zitto Zuberi Kabwe katika JamiiForums ,



Mahojiano ya moja kwa moja na Mhe. Zitto Zuberi Kabwe katika JamiiForums
,

Kama tulivyoahidi tarehe 19/11/2010 katika Jukwaa la Siasa (katika thread hii), leo tumemkaribisha Mhe. Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia CHADEMA, Zitto Zuberi Kabwe kama mgeni wetu rasmi katika mahojiano ya moja kwa moja.

Tunawashukuru wanachama wote walioshiriki katika kutuma maswali ya kumhoji Mkuu Zitto na pia wale wote waliokuwa wakifuatilia kwa karibu na kusubiri kwa hamu hadi siku ya leo.

Mjadala utaongozwa na AshaDii kwa niaba ya wanachama wa JamiiForums; side comments zitakuwa kwenye Jukwaa la Siasa, hapa - Side comments: Zitto in JF Exclusive Interview on the 22nd of November, 2012

*Kwa wenye access ya kuweza ku-post kwenye forum hii ya Great Thinkers, tunaomba msiingilie mjadala; shiriki kwenye link iliyotolewa ya side comments*

Karibuni

Zitto:

Awali ya yote itoe shukrani zangu za dhati kwa kupewa fursa hii adimu ya kuhojiwa na wana JF wenzangu.

Nashukuru pia kwa kuwa ni heshima kubwa sana kwangu maana mimi ni mtu wa pili kufanyiwa mahojiano kama haya baada ya kijana mwenzetu Maxence kama 'founder' wa jukwaa letu. Napenda pia ifahamike kuwa mimi ni mmoja wa wanachama waanzilishi wa jukwaa hili na ninafurahi kuona limekuwa na kwa kweli its a force to reckon with.

Zitto ni Mtanzania aliyezaliwa Kigoma, Kijiji cha Mwandiga. Nimekulia katika kitongoji cha Mwanga, nimekwenda shule ya Msingi Kigoma, Sekondari Kigoma, Kibohehe Moshi, Galanos Tanga na Tosamaganga Iringa. Nimepata Elimu ya Juu Chuo Kikuu cha Zanzibar kwa mwaka mmoja, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Uchumi, Scholarship ya InWent Biashara ya kimataifa na Bucerius School of Law and Business Mineral Economics.

Ninaishi Kijijini Kibingo, Kata ya Mwandiga Wilaya ya Kigoma. Pia Tabata wilaya ya Ilala na Dodoma nyakati za Bunge. Ninaishi na mama yangu mzazi na wadogo zangu.

A. Zitto na Ombwe la itikadi miongoni mwa vyama vya siasa

“ Unalizungumziaje Ombwe la Itikadi Miongoni mwa Vyama vyetu vya Siasa, ambapo tangia mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yaingie nchini, ni vigumu kutofautisha itikadi za vyama vya siasa - kinadharia na kivitendo, hasa ukizingitia ukweli kwamba kwa kila chama, sera na itikadi zinazouzwa au kutekelezwa ni za kiliberali, huku wananchi wengi (hasa vijijini) wakiwa hawana ufahamu juu ya madhara na faida ya itikadi hii ni nini.

- Hii ni changamoto kubwa sana kwa nchi yetu. Itikadi za kisiasa husaidia kunyoosha sera za vyama. Hivi sasa chama chochote chaweza kuwa na sera yeyote ile kwa kuwa hakuna uti wa mgongo ambao ni itikadi. Lazima vyama vijipambanue kwa itikadi zao. Kwa kukosekana kwa itikadi zinazoeleweka vyama vimekuwa kama 'electoral machines' tu. Kukosekana kwa itikadi kunafanya vyama kudandia masuala. Mfano juzi hapa mmesikia Mkutano Mkuu wa CCM umeazimia elimu iwe bure.

CHADEMA tulisema hivi mwaka 2010, CCM wakasema huo ni uwendawazimu kwani haiwezekani. Nakumbuka nilikuwa kwenye mdahalo pale Serena (hivi sasa) mwaka 2010, vijana wa CCM wakaniuliza mtapata wapi pesa za kusomesha watu bure. Nikawajibu kama tuliweza kuwasomesha bure kwa Tumbaku, Kahawa na Pamba, tutawasomesha bure kwa dhahabu, tanzanite nk. Leo CCM wanasema elimu bure. Nimemsikia Lowassa juzi anasema inawezekana. Lowassa huyu nilibishana naye sana mwaka 2010 akisema haiwezekani. Huu ni ukosefu wa itikadi sahihi.

Sababu kubwa pia viongozi wetu hawasomi na hivyo bongo zao hazipo 'sharp' kuweza kuona ni mwelekeo gani wa itikadi wa kufuata. At best tunaimba kama kasuku itikadi zilizoendelezwa nje, hakuna originality.

“Unaiongeleaje sera ya Majimbo ya CHADEMA?

- Ni utekelezaji wa kushusha madaraka mikoani, kupanua uwajibikaji na kuleta maendeleo kwa wananchi. Sera hii ya utawala ndio suluhisho la masuala mengi ya uwajibikaji hapa nchini. Kuna haja ya kuwa na DC? Kwa nini wakuu wa mikoa wasichaguliwe na wananchi? Tulipoamua kupendekeza sera hii kwa wananchi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 tuliambiwa sisi tuna lengo la kuleta ukabila nchini. Inawezekana kuna maeneo fulani fulani tulikosea mkakati. Kwa mfano tulianza kusemea suala hili tukiwa mkoani Kilimanjaro, kwa hiyo CCM ikadakia 'unaona wachaga hawa' sasa wanataka ka nchi kao. Kimkakati tulikosea.

Tulipaswa kuzindua sera hii kanda ya Ziwa au kanda ya Kusini. Tulijifunza kutokana na makosa haya. Hivi tumejiandaa vizuri zaidi kuielezea sera hii. Tunataka kuimarisha Halmashauri za Wilaya/Miji/Manispaa/Majiji kwa kuoondoa nafasi ya Wakuu wa Wilaya na kada nzima pale Wilayani. Majukumu yote ya kisiasa ya DC atayafanya Mwenyekiti wa Halmashauri. Majukumu yote ya Kiutendaji ya Ofisi ya DC atayafanya Mkurugenzi wa Halmashauri. Wakuu wa mikoa wachaguliwe na Wananchi moja kwa moja na wawe na 'executive powers' kwa mambo ya mkoa husika. Tutayaweka kisheria mambo haya. Hii mambo ya Rais kuteua wakuu wa Mikoa nchi nzima hapana. Watu wachaguliwe.

Ninaamini kabisa kuwa Sera hii ikitekelezwa tutaweza kutumia rasilimali zetu vizuri na mikoa itashindana kimaendeleo badala ya kushindana kwa namna walivyompokea Rais mkoani kwao

Unaona tofauti ya msingi kati ya CCM na CHADEMA ni IPI?
- CCM imeshindwa kupambana na adui ufisadi, CHADEMA tunapambana na tutapambana na ufisadi kwa nguvu zetu zote. CCM inaamini katika soko holela, CHADEMA tunaamini katika soko linalojali. CHADEMA inaamini katika nguvu ya Umma, CCM inaamini katika nguvu ya Dola.
“Nini kinakuvutia ndani ya CCM ambacho hakipo CHADEMA?”

Sijakiona bado

“Bado unafikiri wewe kuwa CHADEMA ni tija kwa jamii kuliko kuwa Chama kingine mfano CCM?

- Jamii imefaidika sana na kuwa kwangu CHADEMA. Kupitia Bunge na nje ya Bunge nimeweza kuisimamia Serikali kwenye mengi na hasa masuala ya rasilimali za Taifa kama madini na kufanikiwa kupata sharia mpya ambayo imetoa fursa kwa Watanzania kufaidika na utajiri wao wa madini. Mengi sana ninayofanya nikiwa CHADEMA nisingethubu kuyafanya ningalikuwa CCM.

“Unalizungumziaje suala la kuwa na utitiri wa vyama vingi vya siasa vinavyokula pesa za walipa kodi halafu havina tija wala mchango wowote kijamii zaidi ya kutufilisi, je kuna umuhimu wa kuifanyia sheria mabadiliko ili kuwe na limitation mfano, vyama vitatu tu?

Ndio Demokrasia.

Tusiminye kabisa watu kuwa huru kuanzisha vyama vya siasa. Baada ya muda ni vyama vyenye uwezo wa kukonga nyoyo za wananchi ndio vitabakia. Wala hatuna haja ya kuweka sheria. Huko mbele ninaona Tanzania yenye vyama sio zaidi ya 4. Vyama vikubwa 2, CCM and CHADEMA. na CUF watakuwa a balancing party kama ilivyo LibDems UK au Greens and Liberals Ujerumani. Kwa hali ya sasa ya muungano ninaona kuwa CUF yaweza kuwa kama The Bloc Québécois ya kule Canada. Sioni NCCR ikidumu. Soini future ya UDP bila Cheyo na TLP bila Mrema.

Lakini pia kuna uwezekano mkubwa sana wa Kundi moja la CCM kuunda chama kingine cha siasa ambacho kinaweza kuwa na nguvu hata zaidi ya CHADEMA. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 tutaona hivi new configurations. Tuache watu wawe huru kuunda vyama. Vyenye nguvu vitabakia


B. Zitto na CHADEMA

Nini kipaumbele chako cha sasa kama mwanachama wa CHADEMA?
- Kutumikia chama chetu kwa nafasi nilizonazo.

Natumia nafasi yangu ya Ubunge na Uwaziri kivuli kuhakikisha kuwa chama kinapata taswira chanya mbele ya jamii, Na kinaleta mabadiliko ambayo chama tawala, yaani CCM, kinashindwa kuwafikishia wananchi. Utaona kwamba, kama unafuatilia Bunge, hakuna mkutano wa Bunge unaopita bila hoja mahususi inayojenga taswira chanya ya chama.

Ni bahati mbaya sana kuwa hatutumii baadhi ya mafanikio yetu Bungeni kwenye ulingo wa siasa ma hivyo kuwaacha CCM wanachukua credits.

Kwa mfano, ni kwanini mafanikio ya hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu hatujayafanyia kazi ya kisiasa? Ingawa hatukufanikiwa kumtoa Waziri Mkuu lakini tuliilazimisha Serikali kufanya mabadiliko. Kikwete alisema ni upepo tu, lakini upepo huu ulikuwa na joto kali ukamshinda na tukaacha yeye achukue credit kwa kazi yetu ya uwajibikaji.

Hoja ya juzi ya Mheshimiwa Halima Mdee kuhusu Ardhi inabidi kuifanya ni ajenda ya kisiasa. Hoja ya Mkonge tulikwenda Tanga na ilikuwa na mafanikio makubwa sana. Hoja ya Mabilioni ya Uswiss nayo tunaiachia wanaisemea watu wa CCM kuififiza. Historia inatuonyesha kuwa hoja zote tulizozitumia vizuri nje ya Bunge zilijenga taswira nzuri ya chama ie Buzwagi na EPA.

We ignore this at our own peril

Mkuu, ni kweli kuwa CHADEMA ni chama cha kidini/kikabila? Na kama ni kweli, tatizo hilo lishughulikiwe vipi? Kama si kweli, unaweza kuueleza umma wa watanzania una kauli gani juu ya mitizamo hii dhidi ya chama chenu?

- Chadema ni chama cha kitaifa. Kingekuwa chama cha kidini au kikabila kingefutwa. Katika uongozi wa Chadema unapata watu toka mikoa na kabila mbali mbali, pia watu toka dini mbali mbali. Diversity hii haipatikani katika vyama vingi humu nchini. Nadhani mtazamo huu unapandikizwa na watu ambao hawakipendi chama chetu na wanao ona chama kama threat kwa maslahi yao binafsi.

Pia sisi kama chama tunapaswa kuwa makini sana, hasa viongozi tunapofanya kazi zetu ili kutothibitisha taswira hii mbaya dhidi ya chama chetu. Baadhi ya wanachama wa CHADEMA ndio mabingwa wa kueneza jambo hili. CCM nao humo humo wanapandikiza mbegu za chuki. Unakuta Waziri wa CCM anamwita Mbunge wa CHADEMA na kumwambia, fulani bwana mdini sana. Mwangalieni. Kiongozi wa CHADEMA anajiona kapata bonge ya issue na kueneza. Tunachinjwa na CCM kwa upuuzi wetu. Kwa ujinga wetu wenyewe. Chama chetu kimesambaa nchi nzima na viongozi wake ni wa dini zote na makabila yote.
“Mh. Zitto, unaizungumziaje demokrasia ndani ya chama chako katika chaguzi, teuzi na kupanga safu za uongozi?”

CHADEMA ina demokrasia ya aina yake na wanachama tunaridhika nayo. The Party deploys for or against your wishes and every member must oblige a just deployment. Tuna utaratibu mzuri sana wa kujieleza na kutetea hoja zetu ndani ya chama, na baada ya watu wote kukubaliana tuna hakukusha tunasimama wote kwa kauli moja sehem zote tunapo wakilisha chama. Sio katika kupanga safu za uongozi tu, ni sehem zote za uongozi wa chama.
“Kwanini CHADEMA haiwatumii viongozi wa Mikoa na Wilaya na badala yake inatuma watu toka makao makuu hata kwa mambo madogo madogo ambayo yangemalizwa na uongozi wa ngazi husika?

Huo mtazamo unaweza kutokana na kulinganisha Chadema na vyama vingine. Ieleweke kua Chadema ni chama tofauti na kina utaratibu wake. Katika chama chetu Viongozi wa mikoa na wa wilaya wana majukumu yao, na makao makuu pia yana majukumu yake.

Inaweza kutokea mara kwa mara hizi level mbili zishirikiane katika kutekeleza kazi za chama. Hata hivo, tunaendelea kujenga chama kama taasisi, hivyo tunaendelea kujenga uwezo wa viongozi wetu wa mikoa na wilaya ili waweze kumudu majukumu mengi zaidi na kuwaachia wenye kukaa makao makuu kuhusika zaidi na strategies za chama.

“Mh Zitto, unazizungumziaje harakati za M4C na athari (impact) yake kisiasa na kijamii? Chama kimeweka taratibu gani nzuri za malezi kwa wanachama wapya wanaojiunga kwenye M4C, kama bado, huku si kusuka kamba inayoungua?”

Kwa sababu jina lake liko wazi kabisa, M4C ni moja ya operesheni inayo fanikisha watanzania kujiunga katika chama huku wakijua kabisa kua malengo ni kuleta mabadiliko chanya.

Impact yake kwa jamii ni kubwa sababu inawaweka wanachama wenyewe kua vyanzo vya mabadiliko. Baada ya kujiunga, ni obvious kua Chama kinatoa mafunzo kwa wanachama wake wapya na hivyo kuwalea kuwa makada wazuri. Hii sio opresheni ya kwanza ya Chama, na haitakua ya mwisho.

M4C sio chama ndani ya chama, M4C ni operesheni ya kujenga chama na kuleta mabadiliko nchini.

Inadaiwa hushiriki kikamilifu M4C, ni kweli? Nini kauli yako dhidi ya tuhuma hizi?
Ninashiriki sana kazi za kujenga chama. Nimeshiriki sana operesheni mbalimbali za chama. Nitaendelea kushiriki nikiwa mwanachama na kiongozi wa chama.

Halikadhalika wengine tunashughulika zaidi katika kuwakilisha chama Bungeni na mikakati mengine ya kuhimarisha chama, ila tukipata nafasi tunajiunga pia katika kazi za kujenga chama. Mikutano yetu ya chama tunagawana maeneo.

Mimi, kwa mfano kwenye M4C nimepangiwa mkoa wa Manayara na Singida nikiwa na Tundu Lissu na Christina Lissu na Rose Kamili. Mtakumbuka mwanzo mwa mwaka nilifanya ziara Tanga bila viongozi wenzangu. Mtakumbuka nilikwenda Marekani kufungua tawi la chama kule. Nimefanya mikutano Iringa, Hanang nk. Nimeshiriki kampeni za udiwani maeneo mbalimbali nchini. Siwezi kuonekana kila mkoa kila wakati. Pia ninapangiwa kazi.
Je, utaratibu wa kupita mikoani katika kutafuta nafasi ya kugombea uenyekiti kama ilivyokuwa wakati wa Mbowe unafaa au CHADEMA irudi katika utaratibu kama wa CCM?
Hatujawahi kufanya utaratibu unaosema isipokuwa kwenye Urais mwaka 2005. Hatujarejea tena utaratibu huo. Mfumo wowote ambao unapanua demokrasia ya chama ni bora zaidi katika kuimarisha chama. Chama kinakomaa kwa wanachama kushindana kwenye chaguzi za ndani. Natumai uchaguzi mkuu ujao wa chama utakuwa na wagombea wengi zaidi ili wanachama wapate uchaguzi wa kweli. Sipendi chaguzi za kupita bila kupingwa katika chama kinachotaka kujenga demokrasia ya nchi.
Mheshimiwa Zitto Viongozi/CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kufichua ufisadi. Kuna taarifa kuwa kuna mwanachama wenu katafuna fedha za M4C, ni kweli? Kama ni kweli, ameshughulikiwaje? Kama hajashughulikiwa, ni kwanini mko kimya?
Nasikia suala hili hapa, tupeni ushahidi na tutachukua hatua mara moja.
Zitto wewe ni naibu katibu mkuu wa CHADEMA, Mara nyingi matamko ya chama yametolewa na Katibu, Mwenyekiti, Mnyika (tangu kabla hajawa msemaji) na mara chache wanasheria km Lissu, Marando na Prof.Safari. Kwanini Zitto umekuwa mbali sana na matamko haya ya CHADEMA ukiwa kama Naibu Katibu mkuu? (Naamini hutojibu ni mgawanyo wa kazi)
Naibu Katibu Mkuu sio msemaji wa chama. Katika kujibu suala la demokrasia katika chama nilisema kuwa kuna utaratibu wa kujadili hoja mbali mbali ndani kwa ndani, yakiwemo matamko ya chama.

Katibu mkuu wa CHADEMA anapotoa matamko ya chama anatoa yale yaliyojadiliwa na wanachama wote, nikiwemo mimi, hivyo kuwakilisha maoni yangu pia. Sidhani kama kuna umuhimu wa kuifanya kazi hiyo wakati nimeridhika kua maoni yangu yanawakilishwa kupitia utaratibu wa chama.
Unafikiri CHADEMA uliyoikuta mwanzo ndiyo hii ya sasa au kuna mabadiliko? Kama kuna mabadiliko ni yepi na unafanya nini kufanya CHADEMA iwe kama ambavyo ulitaka iwe?
CHADEMA ni chama kinachokua kwa kasi sana, na kadiri kinavyokua kinabadilika positively. Moja ya mabadiliko hayo ni idadi ya wanachama, nyingine ni kuweza kushika Uongozi wa Upinzani Bungeni, nafasi ambayo ilikua ya CUF nilipo ingia chama. Chama hivi sasa kipo kila mahala.

Nakumbuka mwaka 2005 tulikwenda Mafinga kuhutubia tukapata watu 20 tu kwenye mkutano. Leo tunaombwa kwenda huko. Chama kina influence maamuzi ya nchi hivi sasa. Hayo yote ni mabadiliko makubwa na mazuri, na ninafurahi kuwa sehemu ya mafanikio ya chama changu.
Unafikiri namna CHADEMA inavyoendesha siasa zake kuna uwezekano wa kushika dola mapema (2015)? Kama ndiyo kwanini na kama hapana unafikiri mabadiliko gani yanatakiwa kufanyika kuelekea 2015?
Sina mashaka na hili. Nitafafanua zaidi baadaye
CCM wanadai kuwa nyinyi CHADEMA hamna presidential materials, una kauli gani juu ya hili?
Kweli unategemea kuwa chama tawala kinaweza kukisifu chama cha upinzani kwa kuwa na presidential material? Mimi ni Presidential material kwa mfano.

Nina Uwezo, Uadilifu na Uzalendo wa kuweza kuwa Amiri Jeshi Mkuu. Dkt. Slaa ni Presidential Material. Mbowe ni Presidential material. Kitila Mkumbo ni Presidential material. Wapo wengi sana ndani ya CHADEMA wenye sifa za kuwa Marais. Sina mashaka kabisa hilo.
Una muono gani kuhusu upinzani nchini na nini nafasi ya upinzani hasa CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ukilinganisha na chama tawala CCM?
Ili Tanzania iwe salama ni lazima CCM ishindwe uchaguzi. CCM ikishinda tena mwaka 2015 itavunja sana moyo wa wananchi na wengine wanaweza kukata tama. Lakini pia CCM imechoka na haina nguvu za kutosha kukabiliana na changamoto za nchi hivi sasa.

Njia pekee ya kuisadia CCM iweze kujipanga upya ni yenyewe kondoka madarakani. CHADEMA ina nafasi kubwa sana ya kushinda na kuongoza dola. Muhimu chama kijipange na kuonekana kama chama kilichotayari kushika dola. Tuyatende tunayoyasema na tujiimarishe zaidi.

C. Zitto na kuhusishwa na CCM

Kumekuwa na shutuma za mara kwa mara kuwa una ukaribu uliokithiri na Chama kuu pinzani kwa CHADEMA yaani CCM. Unasemaje kuhusiana na tuhuma hizo?
Ukitaka kummaliza mwanasiasa yeyote wa upinzani hapa Tanzania mhusishe na ama usalama wa Taifa au CCM. Ndivyo ilivyokuwa kwa Mabere Marando miaka ya Tisini. Marando ameishi kuweka sawa historia ingawa propaganda dhidi yake zilikuwa kali sana kiasi cha kuogopwa kweli kweli. Napita njia hiyo hiyo ya Marando na wanaonipaka matope haya wataona aibu sana ukweli utakapodhihiri.
Siku za mwisho za uhai wake ndugu Chacha Wangwe naye aliambiwa ni CCM na kwa kweli alikufa akiwa na chuki sana kuhusu tuhuma hii.

Faida kubwa niliyonayo mimi ni kwamba, mtaji wangu wa kisiasa ulikuwa ni mkubwa mno na ndio maana tuhuma hizi hazijaniathiri. Ninaamini tuhuma kama hizi zingekuwa kwa watu wengine wangekuwa wameshafutika kwenye historia ya siasa. Sijawahi kuwa mwanaCCM, familia yangu yote kabisa ni waanzilishi wa CHADEMA. Sina historia na CCM. Inawezekana wanaosema mimi ni CCM wengi wao wamewahi kuwa CCM, wana familia zao ndani ya CCM na wamewahi kula matunda ya CCM. Mimi sijawahi na wala sitawahi.
Inasemekana kua ukaribu huo unaweza kuonekana kupitia ukaribu wako na Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni rais wa Jamhuri wa muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete. Unasemaje hapa?
Kuhusu Rais Kikwete, kwanza ifahamike Jakaya Kikwete na Zitto Kabwe wana mahusiano yao nje ya siasa na hata siku moja hatujadili vyama vyetu. Rais Kikwete anaamini katika uzalendo wangu.

Mimi ninamheshimu Rais Kikwete kama Mzee wangu. Kuita sisi ni marafiki is understatement, yeye ni mzee wangu. Tunaheshimiana, lakini ninaiheshimu zaidi Tanzania na ninaipenda zaidi Tanzania. Kama inavyoonekana, kazi zangu zinajihidhirisha Bungeni kwamba ni mmoja wa wabunge ninayeisumbua sana Serikali yake. Kutokana na hoja zangu nimemlazimisha kufanya mambo kinyume na mipango yao. Leo tuna sheria mpya ya Madini kwa sababu ya hoja ya Buzwagi. Ninafurahi sasa mgodi wa TanzaniteOne hisa asilimia 50 zinachukuliwa na Watanzania kutokana na mapendekezo yangu mahususi kwamba vito vya thamani, mgeni asiwe na zaidi ya asilimia 50.

Mwaka huu nimemlazimisha kupangua baraza la mawaziri kufuatia hoja yangu ya kutokuwa na imani na waziri mkuu iliyoungwa mkono na wabunge wengi bila kujali vyama. Hebu niambie kama ningeweza kupata mafanikio kama haya dhidi ya Serikali ya mtu mnayesema rafiki yangu. Wengine watasema, aah JK huwa anamtuma kufanya haya. Iwe jua au mvua ni lawama tu. Lakini maisha ya kisiasa haya. Yana mwisho, Rashidi wa KULI alisema.
Mkuu, vipi kuhusu kuonekana kwako in public pamoja na rais sehemu tofauti hadi safari za nje ya nchi.
Suala la kusafiri na Rais ni suala la kawaida sana. Nashangaa sana namna linavyokuzwa wakati ni wazi kabisa kua Rais lazima asafiri na wabunge, na anae wateua wabunge ni Spika wa Bunge. Kila Rais, Makamu wa Rais au Waziri mkuu wanapo safiri huambatana na wabunge wa kambi zote mbili.

Kwa kuweka rekodi sawa Rais amesha safiri na wabunge wafuatao wa Chadema: Christina Lissu (Australia), Chiku Abwao (Burundi), Grace Kiweli (Scandinavia), Lucie Owenya (US), nk. Makamu wa Rais kesha safiri na Ezekiah Wenje (Uturuki) na Esther Matiko (Uturuki) Waziri Mkuu pia kesha safiri na wabunge wa Chadema.

Toka nimekuwa mbunge nimesafiri na Rais mara mbili tu: Mara ya kwanza ilikua sherehe za uhuru za Sudan Kusini. Nilikwenda kwa taratibu hizo za Bunge. Mara ya pili ni Ethiopia, Kumzika Meles Zenawi. Hii niliomba mwenyewe kwani nilipenda kwenda kumzika mwanasiasa huyu niliekuwa namheshimu sana barani Afrika.
Inasemekana kuwa ni Kwa sababu yako ndio maana rais JK hakumnadi mgombea wa ubunge wa CCM wa jimbo lako katika uchaguzi mkuu uliopita na kwamba ndio maana hukushiriki katika kuungana na wanachama wako katika kumsusia JK siku ile anafungia bunge.
Rais Kikwete hakufika jimboni kwangu kumnadi mgombea wa chama chake. Napenda niwakumbushe, sio mwaka 2010 tu, toka nimekuwa mbunge Rais Kikwete hajawahi kuja kwenye kampeni jimboni kwangu. Hakuna makubaliano yeyote, bali anaheshimu mchango wangu kwenye nchi yangu. Mwaka 2005 hakuja Kigoma Kaskazini. Mwaka 2010 hakuja Kigoma Kaskazini. Lipumba pia hakuja Kigoma Kaskazini kunadi mgombea wake wa CUF.

Mwaka 2005 katika Jimbo la Musoma Mjini, aliyekuwa mgombea Urais CHADEMA ndugu Mbowe, hakumnadi mgombea wa CHADEMA bali alimnadi mgombea wa CUF. Mwaka 2010 Slaa alipofika Kyela alimnadi mgombea wa CCM dkt Mwakyembe. Kama ilivyo kwa wengine wenye maamuzi ya kuthamini kazi za wagombea wa vyama vingine, Rais Kikwete naye anayo haki ya kuheshimu na kuthamini kazi zangu katika nchi yetu. Mwakyembe yupo kwenye majukwaa ya CCM licha ya kwamba alinadiwa na Mgombea Urais wa CHADEMA.
Vipi madai kuwa unatumwa na CCM ili kupunguza nguvu ya CHADEMA? Kama si kweli unadhani kwanini watu wanakuona kama pandikizi ndani ya CHADEMA?
Baadhi ya watu wanapandikiza chuki hizi kwa sababu zao wenyewe. Hawanisumbui maana najua ni kikundi kidogo cha watu wachache wenye malengo yao ovu. Wajue tu kwamba hawawezi kuwadanganya Watanzania ambao wanafanya maamuzi yao sio tokana na propaganda ila kutokana na matendo ya kila mmoja.

Onyo:
Watu hao hawawezi kummaliza Zitto kisiasa bila kuiathiri CHADEMA maana the imaage of Zitto is so intimately intertwined with CHADEMA that you couldn’t attack Zitto without jeopardizing the image of Chadema, and vice versa.

Wanaoeneza sumu hii hawana nia njema wala mapenzi na CHADEMA. Hawaelewi siasa. Wanafurahisha maadui wa CHADEMA. Maadui wanawachochea kwa kuwapa habari za uwongo na wao wanadhani watammaliza Zitto. Huwezi kummaliza Zitto bila kuiathiri CHADEMA. Hawatafanikiwa.
Ni kweli kuwa una mkakati wa kuhamia CCM kabla ya 2015?
Sijawahi wala kufikiria kuhamia CCM. Kama nilivyosema hapo awali, sijawahi kuwa mwanachama wa chama kingine chochote tofauti na CHADEMA. Namwomba mungu kuwa niondoke duniani nikiwa chama hiki hiki. Siamini katika kuhama vyama. Ninaamini katika mfumo imara wa vyama vingi nchini. Ninaamini katika demokrasia pana.
Vipi tetesi kuwa wewe na Kafulila mmeanzisha chama na una mkakati wa kutimkia huko?
Swali hili na lililotangulia yanaonyesha kuwa hizi kweli ni tetesi tu. Sasa kama unasema nina mkakati wa kuhamia CCM. Tena kuna tetesi nimeanzisha chama na nataka kuhamia huko, sasa mimi nina vyama vingapi nitakavyohamia. Sijawahi hata kufikiria kuanzisha chama cha siasa. Chama changu ni CHADEMA na sitaondoka CHADEMA. Kinachonisikitisha ni kwamba kuna viongozi wa CHADEMA wamekula sumu hii na bila woga wanaisema kana kwamba ni kweli.

It is very unfortunate Kiongozi wa chama makini kama CHADEMA kuamini ujinga na kuingia kwenye mitego kama hii. Nataka ijulikane wazi kabisa kwamba, CCM haitachoka kutugawa. Haitachoka kupandikiza chuki miongoni mwetu. Wameshajua udhaifu upo wapi na wahenga walisema kamba hukatikia?

D. Zitto na Kigoma

Unaweza orodhesha utofauti wa Kigoma ya sasa na Kigoma kabla ya Zitto kuwa mbunge wake?
Hili watasema watu wa Kigoma wenyewe. Sio watu wa jimboni kwangu tu bali watu wa mkoa mzima wa Kigoma. Kigoma ya mwaka 2005 na Kigoma ya mwaka 2012 ni sawa na kichuguu na mlima Kilimanjaro. Tunaendelea kusukuma maendeleo zaidi ya Mkoa huu. Nafurahi sana kuwa sehemu ya mabadiliko haya ya mkoa wangu. I am very proud.

Hata hivo naamini bado kuna mengi zaidi yanayo takiwa kufanyika na nitashirikiana na wabunge wetu watakao kuja kuhakikisha Kigoma inasonga mbele. Ni vema watu wa Kigoma watoe hukumu yao wao wenyewe badala ya mimi kuanza kubrag hapa. Watasema barabara zilikuwaje na sasa zipoje. Watasema hali ya umeme. Watasema hali ya kilimo cha kahawa. Watasema hali ya elimu na afya. Humu kuna watu wa Kigoma, waseme wenyewe!
Mkoa wa Kigoma unanufaika/utanufaikaje na ukaribu wako na serikali ya Ujerumani?
Sina ukaribu na Serikali ya Ujerumani.
Umeandaa mikakati gani kuhakikisha Chadema inatetea vema hicho kiti chake?
CHADEMA ni chama imara sana Kigoma Kaskazini. Kina mtandao kila kitongoji na kina viongozi mahiri kwenye vijiji. Tunachohitaji ni kupata mgombea mzuri.

Napenda niseme hapa kwa uwazi kabisa. Viti vyote walivyoshinda NCCR Kigoma isipokuwa Kimoja vilichukuliwa na vijana waliokuwa CHADEMA. Kwanini walitoka ni jambo ambalo sote twapaswa kutafakari (wana chadema) maana naona kuna watu wanatoa majibu mepesi sana kuhusu suala hili. Wengine wanadiriki kusema niliwasadia vijana hawa. Sikuwasaidia lakini nilikataa kwenda kufanya kampeni dhidi yao maana matokeo yake ingekuwa ni CCM kushinda kwa sisi wapinzani kugawa kura.

Kuna wenzangu wangependa bora CCM ishinde kuliko mtu kama Kafulila kushinda, nilikataa nadharia hiyo. Hivi sasa Kigoma ina wabunge wa upinzani 5 kati ya majimbo 8. Wabunge 4 kati ya hao ni wana CHADEMA by nature lakini kushindwa kwetu kuvumulia tofauti zetu kumefanya kuwapa NCCR viti. Ukiangalia kura za Urais Kigoma ilipata asilimia 45 ya kura zote na hata kushinda kwenye baadhi ya majimbo. Lakini tulipata kiti kimoja tu tena kwa mbinde sana. Hili ni somo. Tukijifunza tutashinda viti vyote vya mkoa wa Kigoma bila shida yeyote ile.
Kuna mtu ambaye umemuandaa kugombea nafasi ya Ubunge Kigoma Kaskazini? Ni kwa tiketi ya chama gani? Kama yupo tunaweza mfahamu au bado ni siri kwa sasa? Vipi ndugu Yared Fubusa ana nafasi gani kuelekea 2015?
Sijaandaa mtu. Nachukia siasa za kuandaa watu. Mimi sikuandaliwa kugombea Kigoma Kaskazini. Nilitaka kuwa Mbunge na nikaomba ridhaa. Yeyote anayetaka kuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini lazima aanze sasa kushiriki kazi za chama chetu, tumjue na tumpime na wengine kasha Mkutano Mkuu wa chama katika Jimbo utateua mmoja aliyebora kabisa.

Yared Fubusa ni kijana mzuri sana mwenye maono na mwenye mapenzi ya dhati ya Kijiji chake cha Kiganza na Kata yetu ya Mwandiga na mkoa wa Kigoma. Ninamshauri aanze sasa kushiriki katika kazi za chama chetu cha CHADEMA ili wanachama wamjue na wampime. Anaweza kuwa Mbunge mzuri sana. Nitafurahi kama nitapata mtu wa aina yake kuendeleza jimbo letu. Yeyote anayetaka Ubunge Kigoma Kaskazini ajitokeze sasa. Mimi sitaandaa mtu yeyote. Nataka, kama mpiga kura, tupate mtu safi.
Mgodi wa chumvi wa Uvinza uliouzwa kwa bei ya hisani kwanini hawalipii yale maji ya chumvi ambayo yapo ardhini toka kugunduliwa kwake miaka ya 1800's ("Brine") kwa kutumia "flow meter" kama mwananchi wa kawaida wa Kigoma Mjini ambaye analipia maji ya KUWASA kutoka ziwa Tanganyika? Je, wawakezaji hao waliuziwa hata mkondo wa maji ya chumvi yaliyopo ardhini wakati wao hawakuwa wagunduzi?
Nitafuatilia suala kwenye kamati yangu. Sikuwa nimelitilia maanani.
Pamoja na kuuziwa kiwanda hicho kwa bei ya hisani, kwanini bado wanaendelea kutumia nishati ya kuni kutoka kwenye miti asili ambayo hawakupanda wao badala ya kutumia nishati mbadala?
Ndugu Kafulila anafuatilia suala hili kwa kina sana. Kuna kazi inaendelea hivi sasa kuhusu suala hili sipendi tuiseme hadharani.
Katika vipindi vyote hivi vya ungozi wako wananchi wa Kigoma Kaskazini ungependa wakukumbuke kwa lipi?
Ufahari wa Utu wao. Leo watu wa Kigoma hawaoni aibu kujitambulisha hivyo. Haikuwa hivyo miaka ya nyuma. Hili ni kubwa sana kwangu kuliko mamia ya kilometa za barabara au makumi ya megawati za umeme au Uwanja wa ndege wa Kimataifa.

E. Zitto na Maoni juu ya Tanzania

Nini ni Dira ya Kabwe Zuberi Zitto kwa Tanzania?
Tanzania ambayo kila Mtu ana fursa sawa ya kujiendeleza na kuliendeleza Taifa bila vikwazo vyovyote. Tanzania yenye heshima mbele ya Mataifa ya dunia, wenye watu wanao thamini Utu wa binadam wote duniani, yenye watu werevu wanao tambulika nyumbani na kimataifa, na wenye siha njema. Mwono chanya kuhusu nchi yao na majirani wao. Napenda kuona Taifa imara na bora barani Afrika. Taifa lisilo na taswira ya ufisadi. Taifa la kujivunia. Inawezekana.
Kama leo ungechaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya katiba ya sasa ukiwa amekuta maadui wale watatu (ujinga, umaskini na maradhi) wakineemeka hasa wakiwa wamepata mwenzao ufisadi, ungetumia jeshi gani/mbinu gani kupambana na maadui hawa?
Kwanza kuibadili Katiba hiyo ingekuwa suala la kwanza maana huwezi kupambana na ufisadi kwenye Katiba ambayo ni mbaya.

Pili ningeimarisha sana miiko ya uongozi na kuweka bayana kwamba yeyote anayetaka uongozi wa Umma atumikie umma, biashara aweke pembeni. Hata nchi zilizoendelea zinafanya hivi (conflict of interest code). Hii ndio inaimarisha ufisadi.

Tatu, uwazi wa mali za viongozi, uwazi wa mikataba yote ya kunyonya rasilimali na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi.

Ukishaweka misingi hii na hasa misingi ya uwazi na uwajibikaji kazi ya kupambana na rushwa inakuwa rahisi sana. Hivi sasa tunashindwa kwa sababu hao wanaopaswa kupambana na rushwa wao wenyewe wana maslahi na wanazuia mabadiliko. I am anti status quo person all my life and we need just that.

Suala la mgongano wa maslahi nimeliandikia mara kadhaa na hata jana kuna makala kwenye RaiaMwema kuhusu suala hili. Pia niliandika muswada binafsi Bungeni kuhusu suala hili na niliuweka hapa JF napia kwenye blog yangu zittokabwe.com. Hili ni suala linahitaji sana msukumo ni kuondoa ufisadi nchini.
Kwanini Tanzania ni Maskini? Mkakati gani wa anaouona kuwa unaweza kutambua vipaumbele vya kuondokana na umasikini wa Tanzania?
Tanzania ni masikini kwa sababu viongozi wetu wamechagua tuwe masikini. Njia moja kubwa na ilio endelevu ya kutokomeza umasikini Tanzania ni kuwekeza walipo Watanzania wengi na kuwapa fursa za ajira na ujira, fursa za kuzalisha utajiri kwa kuongeza uzalishaji mali.

Umasikini wa Tanzania utaondoka kwa kuwa na Maendeleo Vijijini. Ili kupata rasilimali za kuwekeza vijijini ni lazima kuondokana na upotevu mkubwa wa rasilimali za nchi kutokana na matumizi mabaya (kama posho), ufisadi, wizi na udokozi, pia kuzuia ukwepaji mkubwa wa kodi. Kazi ndio kipimo cha Utu itakuwa ni kauli mbiu muhimu ili kurejesha ‘attitude’ ya kufanya kazi badala ya kuwa Taifa la wanyemelea-kipato (rent-seekers).
Kama kijana, umetembea nchi kadhaa duniani, kwa muono wako ni wapi wananchi, viongozi, serikali na taifa kwa pamoja tunakosea katika kulisongesha gurudumu la maendeleo Tanzania?
Hatuna wivu wa maendeleo. Tumekata tamaa. Hatuna ‘ambition’ za kuacha legacy kama walivyo kina Mahathir, kina Meles nk. Hatuna attitude ya maendeleo. Watu wenye madaraka hawana mawazo mapana, hawaoni mbali., na hawana constancy and consistency katika strategies zao za kuendesha nchi. Ukienda kwenye blog yangu soma a post imagine Tanzania utaona potential ya nchi hii.
Ikiwa ndani ya uwezo wako i.e tuchukulie umepata urais; ni njia gani ambayo unaweza kutumia kufuta na kumaliza Udini ambao unaanza kujidhihirisha kwenye siasa za Tanzania?
Udini ni state of mind. Tatizo Tanzania tumekuwa kwenye state of denial.

Malalamiko ya Udini katika nchi yameanza siku nyingi sana. Njia ni moja tu, Serikali kutoshughulika na masuala ya Dini na viongozi wa dini kutojiingiza kwenye siasa za vyama bila kupoka uhuru wao wa mawazo au wa kujiunga na vyama vya siasa. Ukiwa na Serikali inayotenda haki kwa watu wote bila kujali wana Sali au wanaSwali hapatakuwa na malalamiko haya.

Hii sio mara ya kwanza tunaona vurugu za kidini kwenye nchi. Kwani mmesahau suala la maduka ya nguruwe miaka ya tisini? Mmesahau suala la mwembechai la miaka hiyo hiyo? Mmesahau mauaji ya Arumeru? Muhimu ni Serikali kuwa imara kuhakikisha tunapiga vita ‘chuki’ kisheria na kutenda haki kwa watu wote bila kujali dini zao. Udini ulivyo sasa ni kansa inayotutafuna kidogo kidogo. Nimeshuhudia mwenyewe udini mkali sana wakati wa kampeni mwaka jana Jimboni kwangu ulioendeshwa na dini zote kuu - Waislam na Wakristo kila mmoja kwa mwono wake.

Nimesoma jana makala ya MwanaKijiji kuhusu namna ya kushughulika na suala hili. Kuna haja ya kuzungumza kwa uwazi bila jazba suala hili. Ningekuwa ni Rais leo ningeunda Tume ya Ukweli na Maridhiano kujadili kwa uwazi na mapana yake suala la Udini. Tusipochukua hatua nchi hii itapasuka vipande. Haya mambo ya Gesi na Mafuta haya ndio yatatumika na maadui wa nchi yetu kutugawa.

Tuwe Makini sana. Tusione tu hizi vurugu kwa juu juu. Tuzungumze

F. Zitto na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Tukiachana na hoja juu ya umuhimu wa wananchi wenyewe kuamua, je, wewe binafsi kama mmoja ya hao wananchi, unadhani mfumo upi ni bora ambao utaweza kusaidia pande zote mbili kuhisi zinafaidika na muungano?
Kwanza kabisa niweke wazi kwamba mimi ni muumini wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Shirikisho la Afrika Mashariki na Mwanamajui wa Afrika (Pan Africanist). Lazima tuulinde muungano wetu kwa kuufanyia marekebisho makubwa sana ikiwemo kutoa uhuru mpana kwa pande za Muungano kufanya mambo yao. Muungano wenye Zanzibar na Tanganyika zenye Mamlaka ya kutosha (Kina ndugu Jussa wanasema Mamlaka kamili, ukisema mamlaka kamili ni sawa na kusema hakuna muungano). Baada ya utangulizi huu, ningependa muungano uwe na muundo gani?

Muundo wa Muungano uwe wa Nchi moja, Dola moja, Taifa moja. Serikali tatu. Kuwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye ni Mkuu wa nchi na Mtendaji kwenye masuala ya Muungano tu ambayo yatakuwa machache kama Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Sarafu, Sera za Fedha, Biashara ya Kimataifa, Kodi za kimataifa, usimamizi wa Rasilimali za Taifa, Uraia nk. Zanzibar watakuwa na Waziri Mkuu Mtendaji na Tanganyika hivyo hivyo. Chama chenye Wawakilishi wengi kwenye Baraza la Wawakilishi la Tanganyika kitatoa Waziri Mkuu na kuunda Serikali na Zanzibar hivyo hivyo. Bunge la Muungano litachagua wajumbe wake kutoka kwenye kila mkoa wa Tanzania wajumbe wawili. Maamuzi yataamuliwa kwa zaidi ya nusu ya kura kwa Wabunge kutoka kila upande wa Muungano.

Kwa mtazamo wako kama Zitto, Je unadhani kuna mambo gani yaliyomo ndani ya Azimio la Arusha ambayo bado yanaweza kutusaidia katika kipindi hiki kigumu bila ya kujali itikadi za kisiasa?
- Miiko ya Uongozi.
- Serikali kuwa msimamizi mkuu wa maendeleo ya nchi badala ya kuachia soko kila kitu.
- Msisitizo wa maendeleo vijijini.
Kuna lingine la muhimu katika hili mkuu… Wengi wanaliponda Azimio La Arusha lakini ni mabingwa wa kukimbia kujadili kitu mbadala wa Azimio la Arusha; Wakibanwa, wanakimbilia Katiba Mpya; Hivi ni vitu viwili tofauti; Declarations mbalimbali ni muhimu sana kwa taifa katika kujipanga kimaendeleo. Unadhani kwanini?
-Katiba sio mwarobaini wa matatizo ya nchi yetu. Unaweza kuwa na Katiba nzuri sana lakini fukara tu. Maazimio yanatoa mwelekeo wa nchi kutokana na nyakati. Katiba inaweka tu misingi ya mtajiongoza namna gani na kwa mipaka gani na maono. Azimio kama ilivyo Azimio la Arusha linaweka utaratibu wa kutekeleza katiba
H: Zitto na KATIBA Mpya

Unazungumzia vipi suala la majina wajumbe wa kamati ya kukusanya maoni ya katiba mpya kuchaguliwa na rais?
- Hili halina mjadala tena maana tume imeshaundwa na majina yameshatangazwa. Vyama vilipeleka majina kwa Rais na Rais akateua kutokana na orodha ambayo yama vimepeleka. Hili swali halina tija kwa sasa.
Ni kipengele/vipengele gani katika katiba ya sasa vina mapungufu makubwa zaidi kuliko vingine na una maoni gani?
Katiba nzima ina mapungufu na hivyo tunaandika upya kabisa. Katiba itakayo tufaa ni yenye kulinda maslahi ya taifa, sio vyama au watu binafsi. Katiba hiyo inatakiwa kuweka msingi ya Tanzania tunayo itaka.

Napenda Katiba ambayo itaimarisha sana Uwajibikaji. Kama Katiba ingekuwa ni neno moja tu basi mimi ningechagua neno hilo liwe 'UWAJIBIKAJI' yaani Accountability. Huu ndio msingi wa Taifa kwa wananchi kuwa na uwezo wa kuwawajibisha viongozi na viongozi kuwajibika kwa wananchi.

Ningependa kuona Katiba ambayo inaweka maliasili zote za nchi, zilizopo chini ya ardhi na juu ya Ardhi chini ya mamlaka ya Dola. Katiba Itamke kuwa Madini, Mafuta, Gesi Asilia, Ardhi na vilivyomo ni mali ya nchi na Katiba na Sheria itaweka utaratibu wa kuendeleza rasilimali hizo kwa faida ya wananchi wote.

Ningependa kuona Katiba ambayo inatupa matumaini ya Taifa tunalojenga. Katiba itakayotumikia wananchi na sio wananchi kutumikia katiba.

Napenda kuona katiba itakayoimarisha Utu wa Mtanzania. Katiba itakayoweka misingi ya dhati ya Utu, Uzalendo na Uadilifu wa wananchi kwa Taifa lao na wa viongozi kwa wananchi.
Unakubaliana na dhana ya kuwa Spika wa bunge amekuwa na madaraka makubwa mno hivyo kuna umuhimu wa kupunguza baadhi ya madaraka.
- Spika hana madaraka yoyote. Unaposema madaraka makubwa mno maana yake nini? Kazi ya Spika ni kusimamia mijadala tu Bungeni. Spika sio mtendaji wa Bunge. Jambo la msingi ni kuboresha kanuni za Bunge ili ziweze kuweka uhuru mkubwa zaidi wa mawazo ndani ya Bunge.
Mkuu Zitto, ningependa kujua kitu kingine kutoka kwako. Katika Mabadiliko ya Katiba yanayokuja kuna uwezekano mkubwa wa MAWAZIRI wasitokane na nafasi za UBUNGE. Kwa muono mwingine wewe umetangaza kutogombea ubunge jimboni kwako. Hii inaweza kuchukuliwa kuwa unawinda UWAZIRI kwa kulifikiria hili?
Duh, umewaza mbali hata mimi sikuwa nimewaza hivyo. CHADEMA ikishinda niwe au nisiwe Mbunge ninaamini nitakuwa Waziri ili kuweza kutekeleza mabadiliko tunayohubiri katika harakati.

Nimetangaza kutogombea Ubunge, kwanza kuomba ridhaa ya chama changu kuwa mgombea Urais na hilo lisipowezekana nitakuwa mpiga debe wa mgombea Urais. Sitaki itokee tena yaliyotokea mwaka 2010 ambapo mgombea Urais alibaki mpweke kwani kila mtu alikwenda kugombea Ubunge.
Je, utaratibu wa sasa wa bunge la JMT wa kupiga kura kwa kuuliza wanaosema NDIYO na wanaosema SIYO ni sawa na unakidhi matwaka ya kidemokrasia uendelee au ubadilishwe? Kwanini?
Kuna mashine ya ki elektroniki za kupiga kura ndani ya Bunge. Nadhani tuanze kutumia hizo ili pia kuweka rekodi za wabunge kuhusu kura zao. Itasaidia sana kujua misimoa ya watu kwenye masuala mbalimbali ya nchi.

I: VITI MAALUM:

Nini msimamo wako juu ya uwepo wa wabunge zaidi ya 100 wa viti maalum ambao kimsingi wanaligharimu taifa mamilioni ya fedha?
Naunga mkono mfumo wa uchaguzi utakaohakikisha kuwa vyombo vya maamuzi vinakuwa na uwiano sawia wa wanawake na wanaume. Napinga mfumo wowote wa upendeleo maana inadhalilisha.

Hivyo Katiba mpya ifute mfumo wa viti maalumu na kuweka mfumo wa uchaguzi utakaohakikisha vyombo vya maamuzi vinakuwa na wanawake na wanaume kwa uwiano sawia. Mimi ni muumini wa mfumo wa Uwakilishi wa uwiano (Proportional Representation).

Nchi za scandinavia zina mfumo mzuri sana wa uwiano ambapo viti vya Bunge vinapatikana kutokana na uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata. Sio lazima tufuate mfumo wao, tunaweza kuwa na mfumo mchanyato. Ujerumani wanafuata mfumo mchanyato na kuna wabunge wengi tu wanawake.

Rwanda pia imefanikiwa kuwa na wanawake wengi sana Bungeni ingawa inabidi kuwa makini kufuata mfumo wa Rwanda demokrasia yao ina mashaka kidogo. Hata hivyo kuja jambo la kujifunza.

J: Zitto na matumizi ya vyombo vya usalama wa taifa katika kulinda maslahi ya chama tawala

Kuna taarifa kuwa CCM inatumia vyombo vya ulinzi na usalama katika kuudhoofisha harakati za vyama vya upinzani, na hasa CHADEMA. Mheshimwa Zitto, una mtizamo gani katika hili?
Ni kweli kabisa. CCM inatumia sana vyombo vya dola kumaliza upinzani. Hata hii ya kugawa wanachama na kupakaza matope baadhi ya viongozi ni kazi ya usalama wa Taifa. Wanapandikiza chuki ili viongozi tusiaminiane. Viongozi vichwa maji wasiojua kazi ya usalama wa Taifa wanafurahia mambo haya kumbe wanatumika
Mhe, kuelekea uchaguzi wa mwaka 2010 gazeti la MwanaHalisi lilichapisha mawasiliano ya simu baina yako na ndg Jack Zoka wa TISS, mpaka leo sijasikia sehemu ukikanusha; kwakuwa hakuna kanusho toka kwako, unaweza kutueleza mazungumzo yenu yalihusu nini?
Naomba nikusahihishe kwamba MwanaHalisi walichapisha mawasiliano hayo baada ya uchaguzi. Suala hili nimeshalisemea sana.

Kwanza ni kweli mimi ninawasiliana na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwemo TISS, Polisi, TAKUKURU na hata JWTZ. Kama kuna kiongozi yeyote wa nafasi kama yangu ambaye hafanyi mawasiliano na watumishi hawa wa Umma basi kiongozi huyo hafai kuwa Kiongozi.

I challenge mtu yeyote aseme kama kuna kiongozi yeyote wa vyama vya siasa ambaye hafanyi mazungumzo na watu wa usalama nk. Jambo la msingi ni mazungumzo mnayoyafanya yanahusu nini? Yanahujumu chama? Niliwaambia viongozi wangu wa chama kwenye vikao vya chama kuwa, kama kuna chembe ya hujuma kwa chama kwenye mazungumzo yangu na watu kama Zoka basi nitaachia nafasi zangu zote uongozi kwenye chama na Ubunge. Nikawaambia wale waliosema wanao ushahidi wa mazungumzo hayo wayaweke wazi. Sio MwanaHalisi wala washirika wa MwanaHalisi waliofanya hivyo.

MwanaHalisi ilikuwa inafanya kazi ya siasa za ndani ya chama. MwanaHalisi walikuwa na ajenda yao dhidi yangu. MwanaHalisi waliamua kunimaliza kisiasa. Hata hivyo kwangu mimi hayo yamepita, ni historia.

Mazungumzo yetu yalikuwa yanahusu nini? Yalikuwa yanahusu nchi. Watu wa Usalama wanasema tunawashambulia sana kwenye mikutano yao na wao sio wanasiasa kwa hiyo mara kwa mara wanajaribu kutusihi tusiwazungumze. Tusiwataje taje. Mara zote nawaambia tutawataja pale ambapo wao wanahusika na kwamba hawapaswi kuhusika na CCM maana wao wanapaswa kulinda dola na sio kulinda CCM.

Wakati nipo Mwanza mapema mwaka 2011 palitokea mauaji ya raia yaliyofanywa na polisi kule Arusha, viongozi wetu wakakamatwa. Mmoja wa waliokamatwa ni Mzee Ndesamburo, mzee wa zaidi ya miaka 75 na wakawa wanamweka katika mazingira mabaya, niliwapigia watu Usalama kuwaambia kuwa hayo ni makosa. Wamwache mzee yule na wanataka kumshikilia wamshikilie nyumbani kwake, sheria zinaruhusu.

Wakati mwingine watu wa usalama wana shida zao pia maana wao ni Watanzania kama sisi.

Kwa mfano, Mwaka 2009 tulikuwa tunapitisha sheria ya Baraza la Usalama wa Taifa. Wakaja kuniomba kuwa sheria ile mbaya na inajaza watu wengi kwenye chombo hicho. Tuka mobilise wabunge kuikataa. Haikukatiza kwenye floor. Mwaka 2008 waliomba sheria yao iboreshwe ili kuondoa kipengele kinachowazuia wao kukamata. Maana sheria ya sasa inasema wao kazi yao ni kushauri tu. Nakumbuka nilifanya kazi hiyo na MwanaKijiji, alinisaidia sana kutafiti na kuandika kwa uzoefu wake wa Marekani kipengele kipya. Hatukufanikiwa na hivi sasa TISS hawana meno!

K: Zitto na wabunge wanaokaa kwenye bodi za mashirika:
Je, unaonaje kama utajiandaa kupeleka ‘Hoja binafsi’ Bungeni ili Bunge liazimie kwamba ni marufuku kwa Wabunge kuwa Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika ya Umma? Sina hakika kama Wabunge watakubali kwa kuwa ni wanufaika lakini kama utapeleka hoja yako kimahiri sina shaka litakubaliwa.
Ushauri mzuri sana. Lakini suala hili sio tu hoja binafsi, suala hili nimewahi kuliandika muswada binafsi zaidi ya mara 4 Bungeni. Mtu yeyote anayefuatilia Bunge atakuwa anajua kuwa kwenye taarifa zote za Kamati ya Bunge ya POAC tumekuwa tukipeleka maazimio haya kwamba wabunge wasiwe wajumbe wa bodi za mashirika ya Umma. Miswada yangu yote ilipigwa chini isipokuwa nilifanikiwa kwenye muswada wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambapo hoja yangu ilipitishwa na Bunge (sijui hawakujua maana sikupata upinzani kabisa).

Lakini nashukuru kuwa baadhi ya Mawaziri wametekeleza agizo la kamati yetu kuwa Wabunge wasiwe kwenye Bodi za Mashirika ya Umma. Waziri Muhongo Kaunda upya bodi ya TPDC, hakuna Mbunge. Waziri Mwakyembe Bodi ya TPA hakuna Mbunge. Waziri Kagasheki kuna Bodi Kaunda hakuna Mbunge.

Toka POAC ilipoanza juhudi hizi mwaka 2009, kuna mafanikio kidogo lakini tunahitaji kuhakikisha kuwa hili haliruhusiwi kabisa. Wabunge wabaki wabunge tu. Kwa hiyo nashukuru kwa ushauri ingawa tayari ushauri huu nimeshautekeleza sio kwa hoja binafsi, bali kwa muswada binafsi unaotunga sharia. Hivi sasa tuna muswada wa Sheria ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na tumeweka kifungu hicho. Tutafanikiwa kuweka misingi ya utawala bora.

Ni kinyume na misingi yote ya utawala bora wabunge kuwa wajumbe wa Bodi za Mashirika ya Umma.

L: Zitto na posho la wabunge:

Najua msimamo wa Chama chako juu ya posho ni kuzipinga, je Chama chako kinatekelezaje msimamo huo kwa vitendo?
Naomba swali hili aulizwe Msemaji wa Chama Bungeni ambaye ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni. Mimi ninajisemea binafsi. Ninatekeleza msimamo huu kivitendo. Sipokei posho za vikao Bungeni na mahala popote ambapo ninahudhuria vikao kama sehemu ya kazi yangu. ( huu ni mfano wa namna ninavyokataa posho #1 Say NO to Posho! « Zitto na Demokrasia)

Posho za vikao ni wizi wa fedha za umma. Posho za vikao ni moja ya dalili za mfumo unaoitwa ‘rent seeking ’ au Pato-nyemelea. Huu ni mfumo wa kujipatia kipato bila kufanyia kazi. Wabunge wamechaguliwa kwa kazi maalumu na tunalipwa mshahara na marurupu mengine kwa kazi hii. Kulipwa posho ya kukaa kitako ni kujipatia kipato bila kufanyia kazi. Wabunge wanakuwa kama genge la majambazi yanayovamia benki na kuiba! Kwa kuwa mfumo unatoa nguvu kwa wabunge, basi hawatumii silaha, bali wanatumia mfumo kujilimbikizia mali. Sitting allowances ni uporaji.
Je, katika suala hili ulipata ushirikiano wa kutosha toka kwa wapinzani wenzako bungeni?
Ndio maana tulikaa kikao na kuamua kuandika barua kwa Spika ili atupe fomu nyingine za mahudhurio na nyingine za posho. Hajafanya hivyo na mimi siandiki mahudhurio. Mimi kama Waziri kivuli wa Fedha nilikuwa nazungumzia na kutekeleza msimamo wa kukataa posho kama sehemu ya kazi yangu. Ndio mandate yangu. I walked the talk. Wengine watajisemea wenyewe maana mimi sio msemaji wao na wala sio msemaji wa Wabunge wa upinzani.
Je, ulipata ushirikiano wa kiwango gani toka kwa Wabunge wa CCM?
Mbunge pekee wa CCM aliyekuwa na msimamo kama wangu ni ndugu Januari Makamba. Alishambuliwa sana kwenye chama chake lakini alisimama kidete. Nafurahi kuona wabunge vijana kama hawa ambao wanaleta aina mpya ya siasa. Ninamtakia kila la kheri. Ndugu Filikunjombe alinipa moyo sana kuhusu suala hili lakini sikumbuki kama naye aliacha kuchukua posho. But he was on my side all the time. January najua alikataa kuchukua posho. Wengine sijui.
Je, hadi sasa hupokei posho za vikao?
Sipokei posho ya kikao (sitting allowances) na sitapokea posho hiyo katika kipindi chote ambacho mimi ni Mbunge. Nikiwa Rais moja wa uamuzi wangu wa kwanza utakuwa ni kufuta posho za aina hii kwenye Serikali nzima. Nisipokuwa Rais nitamshawishi Rais atakayekuja afute posho hizi na kuelekeza fedha tutakazookoa kwenye kuondoa umasikini vijijini.

M: Umeme na Gesi

Una maoni gani kuhusiana na hali ya umeme nchini kwa wakati huu? Itaichukua Tanzania miaka mingapi kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati ya umeme?
Nimekuwa nikitoa maoni yangu kuhusu suala la nishati ya Umeme nchini toka nimekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya POAC. Suala hili wakati mmoja lilitaka kunimaliza kabisa kisiasa kwani msimamo niliochukua niliamua ni msimamo mzuri lakini haukupendwa na wengi ( Sakata la Ununuzi wa Mitambo ya Dowans: Barua ya Zitto kwa Watanzania ).

Bila nishati ya umeme ya uhakika hatuwezi kabisa kukuza uchumi na kuondoa umasikini nchini. Serikali ikiamua baada ya miaka 3 hatutakuwa na tatizo la umeme. Serikali itulize akili kuhakikisha miradi ya Kiwira, mchuchuma na Liganga na mradi wa bomba la gesi unakamilika. Lakini pia Serikali isiwe kigingi cha players wengine kwenye sekta ya umeme na hasa uzalishaji. Serikali ingejikita sana kwenye kusamabza miundombinu na kuruhusu watu binafsi kuzalisha umeme mwingi. Hata hivyo suala la mikataba ya kununua umeme (PPAs) inabidi kuangaliwa vizuri maana mingi inanyonya nchi. Huko tuendako mikataba yote ya aina hii iwekwe wazi kama njia ya kuepuka ufisadi na kuimarisha uwajibikaji. Tanzania inaweza kuwa net energy exporter in the region. Uamuzi ni wetu.
Pia uliposema mikataba iwekwe wazi, ulikuwa na maana gani? Ulimaanisha ikiwekwa wazi hata sisi wananchi wa kawaida tutaweza kuiona ama ulimaanisha iwe wazi kwa wabunge peke yake?
Mikataba iwe wazi kwa wananchi kuweza kuona wakati wowote. Pia itengenezwe nakala za lugha rahisi ili wananchi wa kutoka kwenye maeneo yenye gesi wajue ni nini haki zao na nini wajibu wao. Uwazi wa Mikataba ni silaha kubwa sana ya kupambana na uporaji wa mali asili ya nchi. Uporaji mbaya zaidi ni uporaji dhidi ya kizazi kijacho. Sitaki watoto wetu waje kwenye makaburi yetu kutulaani bali kutuombea dua. USIRI unalea ufisadi.

Kama ni wabunge peke yake ndio waone mikataba hii, hilo litaleta utofauti gani kwenye bunge ambalo wabunge wake wanapiga kura za maamuzi kutokana na chama na si maslahi ya taifa?
Una maoni gani juu ya sera ya Nishati ya Gesi kutafsiriwa kwa Kiswahili?
Tulitoa kauli kupitia Waziri wetu kivuli wa Nishati kuwa Sera ya Gesi iwekwe kwa lugha ya Kiswahili. Imewekwa. Natoa wito kwa watanzania wajadili na kutoa maoni namna ya kuhakikisha kuwa gesi inakuwa kwa maendeleo ya nchi na sio kwa ajili ya watu wachache.

Kwa ujumla nimeandika sana kuhusu suala la mafuta na gesi. Makala hii ( https://zittokabwe.wordpress.com/tag...-gas-sector-2/) inaweza kusaidia ufahamu wa sekta hii na mwono wangu kama Mtanzania. Pia unaweza kwenda kwenye blog yangu utakuta blogposts nyingi sana kuhusu suala hili.

Napenda kuona Tanzania inakuwa nchi ya kupigwa mfano duniani kwa namna ilivyotumia utajiri wake wa gesi na Mafuta. Sitaki turudie makosa tuliyoyafanya kwenye sekta ya Madini. Nitaendelea kufuatilia kwa karibu sana sekta ndogo ya gesi na nitakuwa muwazi sana ili kuzuia 'a nigeria' in Tanzania.

N: Zitto katika Uongozi/Ubunge na Urais 2015

Naomba kujua ni kwanini hasa umekuwa na uamuzi wa kuachana kabisa na Ubunge na kutogombea tena; na kama hayo ni maamuzi yako na hujaeshinikizwa na kitu ama mtu yeyote. Je utaendeshaje maisha yako ya kisiasa nje ya Bunge na nje ya taasisi ya Urais?
Wakati nagombea Ubunge mwaka 2005 niliwaambia wapigakura wangu kuwa nitakuwa Mbunge wao kwa vipindi viwili tu. Niliwaambia nina ndoto za kuja kuwa Rais wa nchi yetu baadaye. Hivyo haya ni makubaliano yangu na wapigakura wangu. Nia yangu ni kupisha wengine nao wakimbize kijiti cha maendeleo ya Jimbo letu na Mkoa wetu. Nimesema mara kwa mara kwamba ukiachana na siasa kazi ninayoipenda zaidi ni ualimu. Nitakapomaliza Ubunge na Urais nitakwenda kufundisha. Ninajiandaa vilivyo kwa suala hilo. Nitapenda kufanya tafiti, kusoma, kuandika na kufundisha. Hivi sasa tunaandaa mpango wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Ziwa Tanganyika (Lake Tnaganyika University) mkoani Kigoma. Nitafurahi kama nitakuwa mmoja wa wahadhiri wa mwanzo wa chuo hiki kufundisha Watanzania Uchumi wa Rasilimali.

Sina wasiwasi pia wa kuendesha maisha maana mimi ni mwanachama wa NSSF, ninajichangia kwa hiari toka nilipoacha kazi katika Shirika la FES mwaka 2004. Ikifika mwaka 2015 nitakuwa nimetimiza ‘points’ za kulipwa pensheni. Nashukuru kwamba nilikwepa ushawishi wa kujitoa kwenye mafao. Naamini nitaendesha maisha yangu kwa kazi za kufundisha, kuuza vitabu, consultancies na pensheni niliyojiwekea akiba.
CHADEMA kina utaratibu gani wa kutangaza nafasi za wagombea katika ngazi mbali mbali hasa ya urais?
Chama chetu hakina utaratibu wowote hivi sasa wa kutangaza nia za watu kutaka kugombea nafasi yeyote. Juzi tumekutana Morogoro na kukubaliana kuwa tutatengeneza utaratibu wa watu kutangaza nia zao wanapootaka kugombea nafasi yeyote ya uongozi. Nadhani huu ni uamuzi mzuri wa chama maana kuna watu wana wasiwasi usio na msingi kabisa kuwa kuwa na wagombea wengi kwenye chama ni kuvuruga chama. Lakini watu hao hao wanashangilia kweli wakiona demokrasia inavyotekelezwa kwenye nchi nyingine kama Marekani. Watanzania wanapenda kuona demokrasia inatekelezwa lakini wanaogopa kuitekeleza wao. Uamuzi wa Morogoro kuhusu mwongozo kwa wagombea utatusaidia sana kuondoa mashaka kama haya.
Katika moja ya ‘school of thought’, inasemekana umetangaza haraka nia ya kugombea Urais kwa misingi ya kuwa Dr. Slaa hana tena mpango huo na kwamba nje ya Slaa huoni zaidi yako ambaye anaweza wakilisha vema. Unalizungumziaje hili mkuu?
Slaa hakuwahi kutangaza nia ya kugombea Urais wakati wowote ule wa maisha yake. Mwaka 2010 Tulimwomba kama chama. Chama kinaweza kumwomba tena na tukifikia mwafaka ndio atakuwa huyo na sote lazima tumwunge mkono. Mimi nimetangaza kwa kuwa ninautaka Urais na hivyo nakiomba chama kiniteue. Pia chama kina viongozi wengine wazuri tu. Tundu Lissu na Mnyika wamesema hawautaki Urais. Ndugu Mbowe yeye hajasema kama anautaka au la. Kumbuka hata mwaka 2005 Mbowe tulimlazimisha, yeye alitaka aendelee kuwa Mbunge wa Hai. Sisi tukamwambia kuwa lazima abebe chama. Nakumbuka mimi binafsi niligombana naye maana aliposema yeye atagombea Hai, nikamwuliza kwa chama gani? Maana kama hutaki kukibeba chama kwenye Urais tutachukua kadi yetu. Ndio! Nilimwambia hivyo kwenye secretariat ya chama. Akakasirika kweli, lakini baadaye alinielewa na mafanikio tuliyoyapata ni makubwa sana baada yeye kugombea. Kwa hiyo hiyo School of Thought ni hisia tu za watu. CHADEMA ina watu wengi sana wenye uwezo wa kuwa maRais. Kitila Mkumbo mnamwonaje? Au mpaka watu wawe Bungeni. Huyu ni hazina ya chama na nchi. Chama kinaweza kusema, Zitto hapana, mwunge mkono Kitila. Nitafanya hivyo. The Party deploys for or against your wishes and every member must oblige a JUST deployment. I will.
Ikitokea kuwa hujateuliwa na chama chako (CHADEMA) kugombea Urais 2015 kwa tiketi ya chama hicho, una nia ya kutafuta chama kingine kitakachokuruhusu kugombea nafasi hii ya Urais?
Nisipoteuliwa na chama kugombea Urais nitamfanyia kampeni mgombea atakayeteuliwa na chama. Siamini katika kuhama vyama ili kutimiza malengo ya kisiasa na ndio maana mimi sijawahi kuwa chama kingine chochote zaidi ya CHADEMA maisha yangu yote. Mwanasiasa anayehama vyama ili kupata uteuzi anafuata vyeo na sio muumini wa sera ya chama husika.Vile vile Urais kwangu mimi sio an end in itself, it is a means ya kuleta mabadiliko ya hali ya maisha katika nchi yetu. Kama ilivyokuwa kwa Ubunge, ambapo nimehudumia wananchi na kuleta mabadiliko makubwa sana ndani ya muda mfupi na sasa nataka kuachia wengine, Urais nao ni hivyo hivyo, kutaka kufanya transformation ya nchi yetu, radical transformation katika uchumi, siasa na jamii. Nataka kuionyesha dunia kuwa tunaweza kuondokana na umasikini in our life time. Sasa kama chama kina mtu mwingine mwenye mwona kama huu, mimi nitamuunga mkono na kumsaidia kuifanya kazi hii.

Kabla ya uchaguzi wa 2010 ulishawahi tangaza kutogombea tena ubunge 2010; ni kitu gani kilifanya ubadilishe huo msimamo?
Mwaka 2009 niliamua kuwa ni bora niache ubunge ili nifanye shahada yangu ya uzamivu na kasha nifanye machapisho. Unajua niliingia Ubunge nikiwa na umri wa miaka 29 tu. Kazi niliyofanya kwenye Bunge la Tisa ilikuwa inanizidi kimo kwa kweli. Nilikuta Bunge limelala sana. Lilikuwa Bunge la status quo. Halikuwa Bunge vibrant kabisa. Siku ya kwanza tu nimeingia Bungeni sikulipenda. Hamu iliniisha. Lakini nikasema ngoja nibadili modus operandi ya Bunge. Nikaanza kutoa hoja kali kali Bungeni na hatimaye nikasimamishwa Bunge. Nafurahi kwamba Wabunge wengine walifuata kasi yangu. Mnakumbuka kuna wabunge walikuwa wanasema ‘hatuwezi kumwachia Zitto Kabwe peke yake kazi ya kuibua ufisadi’ nk. Sasa baada ya kuona nimefanikiwa nikasema basi term moja inatosha. Badaye nikapata ushawishi kuwa hapana, nenda Geita au Kahama au Kinondoni. Nikafanya utafiti wangu nikaona mwenyewe kuwa niende Geita. Viongozi wa chama kutoka Geita wakaenda kuwaona wenzao Kigoma wakakataliwa. Wazee wakanikumbusha kuwa, makubaliano yetu yalikuwa mihula 2. Ikabidi nitimize ahadi hiyo ya mihula 2. Haikuwa matakwa yangu. Mpaka sasa nime abandon PHD yangu maana sina muda na siasa zangu mimi huwa naacha kila kitu kinacho weza kuni divert, hivyo nakosa muda wa kusoma na kuandika.
Tokana na kauli yako hivi karibuni kuhusu kwamba Uongozi wa nchi hautakiwi kuwa mikononi mwa watanzania waliozaliwa kabla ya uhuru; Je kulikuwa na ulazima kutamka haya? Huoni kwamba iwapo utafanikiwa kuwa rais wa nchi yetu, urais wako unaweza kuja kutuletea generational conflicts (misuguano/migongano/mifarakano ya vizazi)?
Mimi ninaamini kabisa kuwa Rais ajaye wa Tanzania ni lazima atokane na kizazi cha baada ya uhuru. Nchi inahitaji a fresh start. Misuguano ndio huleta maendeleo. Hebu tazama nchi hii, Asilimia 70 ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 29! Asilimia 65 ya wapiga kura wapo kati ya umri wa miaka 18 – 40. Hili ni Taifa la vijana. Nusu ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 17! Unaweza kusema hili ni Taifa la watoto. Hawa wazee wetu walipokuwa wanachukua nchi walikuwa vijana. Mwalimu alikuwa Waziri Mkuu akiwa na miaka 39, Mzee Kawawa alikuwa Waziri Mkuu akiwa na miaka 37. Waziri Mkuu wakati huo ndio alikuwa Mkuu wa Serikali maana Mkuu wa nchi alikuwa Malkia wa Uingereza. Angalia mafanikio ya Mwalimu Nyerere na Kawawa kati ya mwaka 1961 na 1971 halafu pima na baada ya hapo mpaka wanastaafu. Tusibwabwaje tu bila evidence. Ndio maana leo Marekani Rais wao ni kijana. Uingereza Waziri Mkuu wao kijana ingawa mataifa haya yana wazee wengi zaidi kuliko sisi. Ninaweza kutamba kwamba mimi ni mmoja wa wanasiasa ambao ninaheshimu sana wazee. Uliza wazee waliopo na waliokuwapo Bungeni ni mwanasiasa gani kijana anatumia muda mwingi nao. Mwulize mzee Sarungi, bahati mbaya mzee Makwetta amefariki. Mwulize dokta Salim, mwulize Mzee Warioba. Wao pia wananiambia, Zitto huu ni wakati wenu. Sisi tulifanya yetu.

Kuna watu lazima watafsiri chochote atakachosema Zitto. Hata hili ninaloandika hapa mtasikia, watasema tu. Kuna watu wanaumwa ugonjwa wa zittophobiasis ni lazima waseme. Mtasikia tu wanasema hivi sasa. Sasa wanaotaka kutafsiri kauli yangu wana mambo yao, lakini ninaamini kabisa kuwa changamoto za sasa za Taifa zinahitaji Rais wa kizazi cha baada ya Uhuru. Wazee watatupa ushauri. This country has to move very fast. We need an ambitous young man, visionery and focused to transform this country. Tunaweza kuwa na Spika mzee ili adhibiti kasi kama inakwenda sana, lakini sio CEO wa nchi. How Old was Lumumba? How old was Kagame? How old is Kabila?

Let us be serious guys. Mnataka tutambae? Wazee wameishi maisha yao. Wameishi yetu na sasa tunataka kuwakopesha maisha ya watoto wetu?

O: Zitto na "Ufisadi na Malimbikizi ya Mali" & "Pesa Uswisi"

Unaposema kuwa ni jitihada zako mwenyewe za kupata hayo majina ya mafisadi wa Uswisi si inakuwa sawa na kuwa una maslahi yako binafsi kama vile kutaka kuyauza hayo majina kwa wale ambao wapo kwenye list?
Nadhani hivi ndivyo ungefanya wewe maana wakati mwingine watu hudhani vyao kwa wengine.
Unachukuliaje mawazo/kauli ya baadhi kuwa kuwasilisha kwako hoja hiyo ya fedha za Uswizi bungeni bila kutaja majina ni moja ya njia ya kujisafisha katika uvumi/tetesi ya kuwepo katika list hiyo ya wenye fedha Uswizi?
Kwangu mimi suala hili ni pana na majina ni sehemu tu ya suala hili. Nimeshasema mara kadhaa kwamba, nina akaunti mbili hapa nchini, CRDB na NMB. CRDB kwa ajili ya mshahara wangu na NMB kwa ajili ya fedha za kujikimu ninazolipwa na Bunge. Sio tu Uswisi, hapa Tanzania sina akaunti benki nyingine yeyote ukiachana na kuwa signatory kwenye akaunti za chama au za kifamilia.

Sina biashara yeyote hapa nchini au nje ya nchi. Naishi kwa mshahara na siwezi kuupeleka mshahara Uswisi. Waliosema mimi nina fedha huko Uswisi walikuwa na lengo la kufifiza hoja yangu kwa malengo yao. Ni watu waliotumwa na usalama wa Taifa au na wenye fedha ili niogope. Watu wa aina hii ni wapuuzi, wapumbavu na hatari sana kwenye vita dhidi ya ufisadi. Tena watu hawa mnawajua na mnawachekea. Hawa watu ni vibaraka wa watu fulani. Tena nasikia wametengeneza na orodha yao ya wenye fedha nje. Hawa ndio wagonjwa wa zittophobiasis. Nasikia wengine walisema kuwa hii hoja akiachiwa Zitto itampa umaarufu. Wapuuzi wanawaza umaarufu tu badala ya kuwaza nchi yetu.

Suala la utoroshwaji wa fedha kwenda nje ni kubwa sana. Tanzania imepoteza dola bilioni 11 toka mwaka 1970 mpaka sasa (ukiongeza na riba kwenye fedha hizo). Halafu kuna wapuuzi fulani wanaleta uzezeta kwenye masuala ya msingi ya nchi. Wanajijua ninaowasema hapa. Waache ujinga. Kama humpendi Zitto basi penda afanyacho kwa maslahi ya nchi yetu.
Kuna ukweli wowote kuwa taarifa ile ya USWISI kuiwekea masharti Tanzania, ilitoka ndani ya serikali ya USWISI au ni mkakati wa mafisadi hawa kuzima jaribio la kurejesha pesa hizo?
Nimetoa kauli jana kuhusu suala hili. Nimesema Watanzania tusiwe mazezeta. Kauli hizi ndio ambazo hata Marekani waliambiwa. Hata Ujerumani waliambiwa. Sisi kuzishabikia badala ya kufanya uchunguzi wetu kwa njia zetu ni dalili za kutaka kuua hoja hii. Hoja hii haitakufa. Tutaisimamia mpaka mwisho.
Je, kuna nafasi ya nchi yetu kufanikiwa kuyarejesha mabilioni hayo ambayo ni kodi ya wanachi?
Tunaweza kurejesha. Kuna Azimio la Bunge na nitahakikisha Azimio la Bunge linatekelezwa. Senegal wanafanikiwa sana. Kenya walifanikiwa kwa kutumia wachunguzi binafsi. Kama Serikali ya CCM itashindwa kufuatilia suala hili, Serikali ya CHADEMA itafanya hivyo. Hawana pa kujificha katika dunia ya sasa.
Ikumbukwe kuwa, tangu nchi hii itumbukie ktk ufisadi mkubwa, chombo chetu TISS kipo kama hakipo, na kama kipo basi ni kwa msaada wa mafisadi tu, Katika mtazamoo na tafsiri ya ripoti yako, taasisi ya Usalama wa Taifa (TISS) Unaiweka katika mizani ipi au haihusiki katika hili?
Idara ya Usalama wa Taifa ni lazima isaidie nchi kwenye masuala kama haya, vinginevyo hawapaswi kuwepo. Sheria ya TISS ya mwaka 1996 inawazuia kuchukua hatua fulani fulani. Tutarekebisha sheria hiyo. CCM wasiporekebisha sisi CHADEMA tutapata ridhaa ya wananchi kuiandika upya sheria ya Usalama wa Taifa. Tunataka usalama wa Taifa na sio usalama wa viongozi au vyama vya siasa.
Kwanini umependekeza kuundwa kwa tume, na kuendelea kumaliza pesa za watanzania wakati kimantiki ripoti yako ilikuwa ni ya kuiwasilisha vyombo vya dola tu, na ikiwa hawajaridhika, TAKUKURU kwa utaratibu wao wa ndani waendeshe uchunguzi na kuchukua hatua?
Uzuri wa Kamati Teule ya Bunge ni kwamba kila kitu huwa wazi kwenye hansards za Bunge na hivyo ni rahisi kufichua uchakachuaji. Pia ngoja niwamegee siasa za Bunge kidogo. Bungeni unapokuwa na hoja unaingia na hitaji kubwa sana wakati unajua fall back ni nini. Tulijua kwa hatua ya sasa hawatakubali kuundwa kwa kamati teule, tulitaka hoja ipite ili kujenga msingi wa kupanua uchunguzi siku za usoni. Tukafanikiwa. Tulitumia approach hiyo hiyo kwenye hoja ya ndugu Halima Mdee. Ni mikakati tu. Sisi tumekuwa ni Bunge la kwanza katika eneo la SADC kutoka na Azimio kuhusu 'illicit money flows'. Sasa tunapaswa kuhakikisha Azimio linakuwa enforced na kisha a public inquiry....
Huku ukijua serikali haina nia ya kuwataja walioficha fedha mabenki ya nje huku wewe ukiwa na majina; unayashikilia hadi sasa ili nini na kwa faida ya nani?
Kwa faida ya uchunguzi. Lazima Serikali ijenge uwezo wake wa kuchunguza na kuweka mambo sawa baada ya uchunguzi. Sasa ikiwa mimi kama mbunge nitatoa jina la walio torosha pesa kwa sasa, nani atatoa majina hapo kesho? Mbunge mpya wa Kigoma kaskazini?
Yale majina ya baadhi ya watanzania unaowatuhumu kumiliki fedha haramu/halali (nyingi) nje ya nchi kwanini huyaweki bayana kwa umma? Wewe kama Mtanzania mzalendo na nchi yako kwanini umeshindwa (na chama chako) kuwapeleka mahakamani na kuwafungulia mashitaka?
Uchunguzi bado unaendelea
Kulikuwa na tetesi kuwa nawe umeficha fedha nje. Hii inaweza kulenga kukuchafua ili uwagwaye waliofanya hivyo, je huoni kuwa hii ni nafasi adimu ya kuondoa shaka? Tuondoe wasiwasi katika hili
Sina fedha za kuficha nje. Nazitoa wapi? Sina biashara naishi kwa mshahara wa ubunge, natoa wapi fedha za kuficha nje?
Kwanini ulipeleka hoja binafsi ndani ya bunge na si kupitia uwakilishi wa upinzani? Je, umefanikiwa kwa kile alichotaraji kutokana na hoja hii? Uliungwa mkono na chama?
Sijaelewa swali lako. Mimi ndio Waziri kivuli wa Kambi ya Upinzani kuhusu Fedha. Upinzani gani tena? Unadhani chama makini kama CHADEMA kinaweza kuacha mbunge wake apeleke hoja bungeni bila kuungwa mkono na chama? Wale wabunge waliosimama kuunga mkono niliposema 'naomba kutoa hoja' ni wabunge wa CHADEMA wale(isipokuwa ndugu Kessy na Kangi Lugola ambao ni CCM).
Vipi, unauongeleaje ujenzi wa bandari ya Bagamoyo?
Ni wazo zuri lakini lifuate mpango wa Ports Masterplan. Sio suala jipya hili.

P: Zitto katika Maswali Mchanganyiko

Nini uelewa wako kuhusu familia? Umeoa? Maana Kuishi au kuwa na mke siyo jambo jepesi, linahitaji uvumilivu na busara nyingi sana, kama vile ilivyo kuishi na mume. Kama hili limekushinda, vipi utaweza kuwaongoza watanzania wote wake kwa waume?
Ninaamini katika familia imara na ni mwumini wa familia ya kiafrika ambapo familia sio tu ni mke, mume na watoto bali pia ndugu na jamaa mbalimbali. Ndio maana ninaishi na ndugu zangu, nimelea wadogo zangu na wazazi wangu na hivi sasa ni nguzo katika ukoo wetu mkubwa sana ambao kuuweka pamoja kunahitaji uvumilivu na busara nyingi sana kuliko hata busara inayohitajika kwa mke na watoto. Mimi sijaoa. Muda ukifika nitaoa. Sitaoa kwa sababu ya kuonekana kiongozi ameoa. Nitaoa pindi nitakaporidhika na huyo mwenzangu ambaye nitafunga naye ndoa. Historia inatuonyesha viongozi wengi sana ambao wameoa na wameshindwa kuongoza nchi zao. Vilevile tuna viongozi wengi sana ambao hawana wake au waume na waliongoza nchi zao vizuri sana.

Indira Gandhi hakuwa ameolewa kipindi chote akiwa Waziri Mkuu wa India. Baba yake Indira, Nehru naye alikaa miaka zaidi ya 30 bila mke. Rais Khama wa Botswana hana Mke wala mtoto, hajapata kuoa lakini anaendesha nchi yake kwa mafanikio makubwa sana kuliko King Mswati mwenye wake zaidi ya 12. Rais Nkrumah alioa mwanamke ambaye hakuwa anamjua akiwa tayari ni Waziri Mkuu wa Ghana, tena aliletewa mke na Rais Nasser wa Misri. Hakuna mahusiano yeyote ya kisayansi kati ya kuoa na uongozi mzuri ingawa kuoa ni muhimu sana. Sidhani kama kuoa itakuwa kikwazo katika uongozi wangu kama itafikia uchaguzi sijaoa maana tumeona viongozi kadhaa wakiamua kuoa baada ya chaguzi. Hata hivyo nitafurahi zaidi kuoa kabla sijawa Rais, lakini ikibidi nitaoa nikishakuwa Rais. Sitalazimisha ndoa kwa ajili ya Urais. Nitaoa nitakapopenda kuoa.
Mkuu Zitto is there any chance unajua mshahara wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mshahara wa makamu wa rais wa JMT, na ule wa rais wa Zanzibar? Ni mahala gani pa kwenda kufuatilia hizo data kwa yeyote yule anayetaka kufahamu hayo? Pia katika hili unadhani ni kwanini hiyo mishahara inawekwa siri sana kwa wananchi hali kimantiki wananchi ndio waajiri wao?
Sijui mshahara wa Rais na naamini ni katika vitu ambavyo walipa kodi wanatakiwa kujua. Mshahara wa Rais hautakiwi kuwa siri kwa mtanzania yeyote. Inapaswa kuwa wazi kabisa na kila Raia ajue. TRA watakuwa wanajua kama sio tax exempt. Nadhani tukifatilia kupitia Utumishi tunaweza kupata hizo data. Hebu ngoja nipeleke swali Bungeni kuhusu jambo hili ili lijibiwe Mkutano ujao wa Bunge. Haya ni mambo ambayo tuna overlook sana.

Mwaka 2008 wakati tunapitisha sheria ya Utawala wa Bunge (National Assembly administration act) niliwasilisha ammendment kuwa mishahara ya wabunge na mawaziri iwe wazi na iwekwe online watu waweze ku access. Nikajibiwa ni siri ya mtu. Rais ni mtu ndio, lakini sio mtu kama mtu mwingine. Ni mtu mwenye maamuzi kuhusu mwelekeo wa Taifa. Ni vizuri kujua tunamlipaje. Ngoja na mimi niwaulize, Nani anajua mshahara wa Mbunge wa Jimbo lake hapa?
Mkuu unadhani unakubaliana na mfumo wa Uongozi wa serikali uliopo sasa? Kama HAPANA unadhani ni mfumo upi ambao ni mzuri na unafaa kwa kupata viongozi wa vyama vyetu kwa ngazi za juu kama M/Kiti, Makamu M/Kiti na Katibu Mkuu – Ule wa kuteua na kupigiwa kura za wajumbe au kugombea na kupigiwa kura na wajumbe na kwanini?
Sina maoni
Ni ukweli kuwa wewe ni mshauri wa uchumi wa Ujerumani. Kama ni kweli, je ni kitu gani kilichokutambulisha hadi kufikia kupewa hiyo nafasi?
Nilikuwa kwenye jopo la Rais Kohler kuhusu Afrika. Nilimaliza kazi hiyo mwaka 2009. Niliteuliwa tu na Rais Kohler wa Ujerumani
Umewahi kuanika utajiri wako (vitu unavyomiliki); unaweza walau kutufafanulia unamiliki magari mangapi, nyumba ngapi n.k?
Nimewahi kusema ninamiliki nini ili kufuta uzushi unaoenezwa kuwa mimi nina ukwasi wa kutisha. Nina gari 2, moja Freelander na nyingine Toyota vista. Ninajenga nyumba Kigoma, kijijini Mwandiga. Nina shamba lenye mikorosho 400 Mtwara, Nina shamba la ekari 3 eneo la Mbutu, Kigamboni. Ninadaiwa na CRDB milioni 120 nilizokopa kwa ajili ya kununua vitu hivyo. Nina mkopo wa Bunge wa kununua gari wa tshs 90 milioni ambao tunalipa nusu yake! Nina exemption ya kodi ya kuingiza gari lakini nimekataa kuitumia kwa sababu mimi kama Waziri kivuli wa Fedha ninapinga tax exemptions na hivyo nimeamua ku walk the talk. Sijaitumia na sitaitumia exemption hiyo.

Nimeamua kuwa ifikapo Mwezi January, mara baada ya kujaza fomu zangu za Maadili na kuziwasilisha nakala ya fomu hiyo ya Mali na Madeni nitaiweka online kwenye blog yangu ili kila mtu aone nimetangaza nina miliki nini na yeyote mwenye mashaka aweze kuniumbua kwa kusema mbona hili umeacha, mbona lile umeacha. Njia pekee ya kumaliza uzushi na majungu ni uwazi. Shaurini wabunge wenu wafanye hivyo pia ili kupambana na ufisadi.
Unazionaje shughuli za kisayansi za watanzania? Je, kuna sera yeyote Tanzania inayompa kijana wa kitanzania nafasi ya kuwa mbunifu?
Kuna sera na sheria za kusaidia ubunifu wa kisayansi. Tatizo ni kwamba Tanzania hatuheshimu sana R&D issues na matokeo yake tumekuwa watumiaji wa ugunduzi wa watu wengine. Kwenye eneo la ICT nimeona vijana wameanzisha The Kinu, tutawasaidia. Hii platform hapa tunayotumia JF imetengenezwa na Mtanzania Maxence, lazima tumsaidie ili iweze kudominate eneo lote la maziwa makuu.